Kambi ya Olunga imani tele ikiendea Ulsan Hyundai

Kambi ya Olunga imani tele ikiendea Ulsan Hyundai

Na GEOFFREY ANENE

WENYEJI Al Duhail, ambao wameajiri Mkenya Michael Olunga, wamejawa imani kabla ya kuvaana na Ulsan Hyundai hapo Jumapili jioni katika mechi ya kuamua nambari tano na sita (mwisho) kwenye Kombe la Dunia la Klabu la mwaka 2020 mjini Al Rayyan, Qatar.

Mabingwa wa Qatar Al Duhail walipoteza pembamba 1-0 dhidi ya wafalme wa Afrika na Misri Al Ahly katika mechi ya raundi ya pili (robo-fainali) uwanjani Education City mnamo Februari 4. Kiungo mshambuliaji Hussein El Shehat alizamisha chombo cha Al Duhail dakika ya 30.

Ulsan kutoka Korea Kusini ilitupa uongozi ikichapwa 2-1 dhidi ya mabingwa wa Amerika ya Kaskazini, Kati na Caribbean, Tigres UANL kutoka Mexico katika mechi nyingine ya raundi ya pili iliyofungua mashindano haya Alhamisi iliyopita.

Kim Kee-hee alipatia Ulsan uongozi dakika ya 24, lakini ulifutwa dakika 14 baadaye na mshambuliaji Mfaransa Andre-Pierre Gignac ambaye aliongeza la ushindi mapumziko yakinukia kupitia penalti uwanjani Ahmed bin Ali.

Mabingwa wapya wa Copa Libertadores (Amerika ya Kusini) Palmeiras watakabana koo na Tigres katika nusu-fainali ya kwanza Februari 7.

Nusu-fainali ya pili itakutanisha Al Ahly na mabingwa wa Bara Ulaya Bayern Munich mnamo Februari 8.

Bayern iliwasili Qatar mnamo Jumamosi jioni baada ya kucheleweshwa saa saba nchini mwao wakisubiri ndege yao kupewa idhini ya kupaa.

Akizungumzia mechi dhidi ya Ulsan, kocha Sabri Lamouchi alikuwa mwingi wa matumaini kuhusu uwezo wa wachezaji wake kupata matokeo mazuri.

“Tumesahau kipigo kutoka kwa Al Ahly na tutaingia mechi ya Ulsan na azma ya kushinda. Kila mtu anatia bidii ili tuweze kupata matokeo mazuri tunayotumainia. Nina matumaini makubwa kuwa wachezaji wangu watajibwaga uwanjani wakiwa wamejaa umakinifu na ari ya kushinda,” aliambia wanahabari.

Al Duhail, ambao wanashiriki mashindano haya kwa mara ya kwanza kabisa, walinunua mshambuliaji Olunga kutoka Kashiwa Reysol zaidi ya majuma matatu yaliyopita kutoka nchini Japan alikoibuka mfungaji bora na mchezaji bora wa mwaka 2020 kwenye Ligi Kuu.  Mchuano wa kutafuta nambari tatu na bingwa itasakatwa Februari 11.

Mgao wa tuzo: Mabingwa Sh1.1 bilioni, washindi wa medali ya fedha Sh440 milioni, nambari tatu Sh275 milioni, nambari nne Sh220 milioni, nambari tano Sh165 milioni, nambari sita Sh110 milioni.

  • Tags

You can share this post!

Wanasiasa wakerwa na matamshi ya Junet Mohamed

Wanaraga wa Machine wazidia nguvu Egerton Wasps