Habari MsetoSiasa

Kambi ya Ruto yapanga njia za kukabili maelewano ya Uhuru na Raila

December 31st, 2018 2 min read

JUSTUS WANGA na IBRAHIM ORUKO

SIKU chache tu baada ya mshirika wa karibu wa Rais Uhuru Kenyatta, David Murathe kutangaza kwamba chama cha Jubilee bado hakijaamua kuhusu mgombezi wake wa kiti cha urais 2022, wandani wa Naibu Rais William Ruto wamebuni mikakati za kukabili maelewano yoyote ya kisiasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Kulingana nao, mbinu hiyo itanusuru azma ya Bw Ruto ya kuwania kiti hicho 2022 na kupunguza kabisa umaarufu wa “handsheki” kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga, ambayo wanahisi imekuwa ikitumiwa kumweka kando Naibu Rais kwa kisingizio cha kuunganisha Wakenya.

Hatua hii kulingana na kundi hilo lililokabidhiwa jukumu la kuhakikisha Bw Ruto anaingia ikulu, itamwonyesha Rais kama kiongozi asiyeaminika na kigeugeu kwa kukiuka makubaliano ya mwaka wa 2013 kati ya vilivyokuwa vyama vya URP na TNA ya kumpokeza Bw Ruto kiti hicho hatamu yake ikikamilika.

“Tulikuwa pamoja katika chama cha Jubilee chini ya kauli mbiu ‘Tuko pamoja’ ila kwa kweli hatuko pamoja sasa hivi. Tulikuwa pamoja na sasa tumetengana. Huwezi kutuambia tuko pamoja ilhali unakula kwenye meza moja na watu waliokupinga,” akasema Kiranja wa Jubilee katika Bunge la Taifa, Benjamin Washiali

Kundi linalopiga ngoma ya Bw Ruto na ambalo limetwikwa jukumu maalum la kuhakikisha anakitwaa kiti cha urais, linajumuisha kiongozi wa wengi kati Bunge la Taifa Aden Duale, mwenzake wa seneti Kipchumba Murkomen, waziri wa kawi Charles Keter, Bw Washiali na seneta wa zamani wa Kakamega, Boni Khalwale miongoni mwa wengine

Kundi hilo linaamini kuwa uwezekano wa kiongozi wao kuchukua urais unadidimia hasa kutokana na kuwa Rais Kenyatta hajamwidhinisha hadharani Bw Ruto kuwa mrithi wake jinsi walivyotarajia.

Suala lingine ambalo limezua wasiwasi katika kundi hilo ni ziara ya majuzi ya Rais eneo la Nyanza ambako alikuwa mwenyeji wa Bw Odinga, jambo ambalo limezua hofu kuwa huenda kuna mwafaka wa kisiasa unaoandaliwa bila kuhusisha Naibu Rais.