Habari Mseto

Kambi za polisi zajengwa katika maeneo yanayolengwa na Al-Shabaab

March 29th, 2018 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

KAMBI za polisi zimebuniwa kwenye maeneo yote hatari ambayo awali yalikuwa yakishuhudia uvamizi wa mara kwa mara kutoka kwa kundi la Al-Shabaab kwenye barabara kuu ya Lamu kuelekea Garsen.

Kamanda Mkuu wa Polisi wa Kaunti ya Lamu, Muchangi Kioi, alisema serikali tayari imeweka kambi za polisi kwenye maeneo ya Milihoi, Nyongoro na Lango la Simba ambako visa vya Al-Shabaab kushambulia msafara wa mabasi ya usafiri wa umma na magari ya walinda usalama vilikuwa vimekithiri.

Bw Kioi kadhalika alisema serikali imeongeza doria za kutosha za polisi na jeshi kwenye barabara kuu ya Lamu kuelekea Garsen ili kuzuia mashambulizi yoyote kutoka kwa Al-Shabaab.

Kamanda Mkuu wa Polisi wa Kaunti ya Lamu, Muchangi Kioi wakati wa mahojiano na Taifa Leo. Picha/ Kalume Kazungu

Aliwataka wasafiri wanaotumia barabara hiyo kuondoa shaka na kusema kuwa usalama wao umedhibitiwa vilivyo.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Al-shabaab wamekuwa wakilenga mabasi ya usafiri wa umma na magari ya polisi na kuyashambulia kwa risasi na mabomu ya kutegwa ardhini.

Watu zaidi ya 30 walipoteza maisha yao kwenye maeneo ya Nyongoro, Milihoi na Lango la Simba baada ya magari waliyokuwa wakisafiria kushambuliwa na Al-Shabaab.

Maafisa wa usalama wakishika doria karibu na msitu wa Boni uliokaribiana na barabara ya Lamu-Garsen. Picha/ Kalume Kazungu

Bw Kioi aidha alisema tangu kambi hizo za polisi kubuniwa, visa vya mashambulizi ya Al-Shabaab havijashuhudiwa tena kwenye maeneo husika.

“Tumeweka kambi za polisi kwenye sehemu za Milihoi, Nyongoro na Lango la Simba. Hizo ni sehemu hatari ambazo zilikuwa zikitumiwa na Al-Shabaab kutekeleza mashambulizi dhidi ya magari ya usafiri wa umma, yale ya kibinafsi na pia yale ya walinda usalama.

Ningewasihi wanaotumia barabara kuu ya Lamu kuelekea Garsen kuondoa shaka kwani usalama umedhibitiwa vilivyo,” akasema Bw Kioi.

Kamanda huyo aidha aliwasihi wasafiri kwenye barabara hiyo kutii amri ya walinda usalama na kukubali kukaguliwa kila wakati wanapofikia vizuiozi vya polisi.

Kamanda Muchangi Kioi akiandamana na maafisa wengine wa usalama kutekeleza doria kwenye msitu wa Boni na karibu na barabara ya Lamu-Garsen. Picha/ Kalume Kazungu

Kamanda Muchangi Kioi akiandamana na maafisa wengine wa usalama kutekeleza doria kwenye msitu wa Boni na karibu na barabara ya Lamu-Garsen

Kadhalika aliwataka madereva kutii amri ya kusafiri kwa mpangilio katika msafara mmoja unaosindikizwa na maafisa wa polisi.

“Kuna baadhi ya wasafiri ambao wamekuwa wakikashifu vizuizi vya polisi barabarani. Wengine wanakataa kupekuliwa. Kuna haja ya wasafiri kutii amri hiyo kwa manufaa yao,” akasema Bw Kioi.