Makala

Kamera inayonasa picha safi gizani kwa umbali wa kilomita moja

May 16th, 2019 3 min read

NA FAUSTINE NGILA

WAKATI Taifa Leo Dijitali ilihudhuria maonyesho ya kiteknolojia katika hoteli ya Radisson Blu, Nairobi, ilikutana na kampuni nyingi, za kimataifa na humu nchini, zilizofika kuonyesha teknolojia za kisasa.

Katika maonyesho hayo ya East Africa Com ya mwaka huu, mada ilikuwa ‘Kueneza mageuzi ya kidijitali ili kuimarisha uchumi wa mataifa ya Afrika Mashariki.’

Maonyesho hayo yalikariri haja ya ushirikiano baina ya kampuni za mawasiliano, habari na teknolojia kuwaunganisha watu wa jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kampuni tajika zilizofika kutoa maelezo ya teknolojia zake ni Canon, Diksha, Ekinops, ECI, PCCW Global, Mediatek, CSG, Hudaco, Icolo, Thuraya, TDii, BotLab, Teledata Solutions, Talinda East Africa miongoni mwa zingine.

Zilikuwa na ubunifu wa kisasa kuhusu upigaji picha, ulinzi na usalama mitandaoni, blockchain, suluhu za mitandao, upeperushaji wa habari na data, teknolojia za kilimo, fedha na setitaiti.

Tulivutiwa na onyesho la kampuni ya unasaji wa picha na video za kidijitali Canon, ambayo iliweka skrini kubwa kwa wapenzi wa teknolojia kutazama huku wameduwaa.

Meneja wa mauzo wa kampuni hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati Bw Parag Kauangal alitukaribisha kwa kituo chao kwa tabasamu.

“Tunalenga kuwaonyesha ubunifu wetu wa kisasa kuhusu kamera na mashine ya kupiga chapa ambazo zinadhamiria kuziba mwanya mkubwa uliopo katika usalama wa mali ya kampuni nyingi na pia mbuga za wanyama,” alisema.

Raul Gabat, ambaye ni afisa wa mauzo, alikuwa hampumziki huku akijibu maswali ya wanateknolojia. Alikuwa ameweka kamera mbili za kisasa ambazo zimewalazimu watazamaji kumsikiza kwa makini.

Mojawazo ni Canon ME20F-SHN ambayo imeunganishwa na skrini ili kuelezea uwezo wake, na nyingine ni  Canon XF705.

Ameweka kisanduku cheusi kati ya kamera ya ME20F-SHN  na skrini. Anawasha mwangaza ndani ya kile kisanduku kisha kuwaagiza watu kuchungulia ndani kupitia kishimo. Wanapoona picha zilizomo mle ndani anazima na kutia giza ndani.

Sasa anaiweka lensi ya kamera hiyo katika kile kishimo. Kila mtu anashangaa kwa kuwa picha zinazotokea kwenye skrini ziaonekana vizuri licha ya kuwa na giza mle ndani.

“Kamera hii inaweza kutumiwa kwa manufaa ya kumulika wezi wakati wa giza, hasa usiku ambapo wanapenda kuiba. Watashawishika hakuna anayewaona lakini kamera hii itakuwa inawarekodi ni kana kwamba ilikuwa mchana wa jua,” anaeleza.

Ni kamera inayoweza kuunganishwa kwa intaneti na huweza kumtambua mtu akiwa umbali wa kilomita moja kwa rangi, ndani ya giza. Ni kamera isiyotumia kifaa cha mwanga wa kamera kumulika inachorekodi, na inatumia teknolojia ya infrared ya kisasa.

Kupitia teknolojia hii, majangili na wawindaji haramu kwenye mbuga za wanyama wanaweza kunaswa na nyuso zao kutambuliwa na kutumika kama ushahidi mahakamani baada ya kutuma polisi kuwakamata. Ni teknolojia ambayo ina uwezo wa kulinda wanyamapori na kukuza uchumi wa nchi.

Bw Gabat sasa aligeukia kamera aina ya Canon XF705 inayorekodi video huku akisema ndiyo kamera ya usoni.

Kutoka kushoto: Meneja wa mauzo Afrika Mashariki na Kati wa Canon Bw Parag Kauangal, afisa wa mauzo Bw Raul Gabat na meneja wa biashara endelevu Bw Ameur Allag waonyesha kamera ya kisasa ya Canon ME20F-SHN inayonasa video safi kwenye giza totoro. Hpa ni katika hoteli ya Radisson Blu, Nairobi ambapo maonyesho ya teknolojia ya East Africa Com yalifanyika Mei 14 na 15, 2019. Picha/ Faustine Ngila

Ikiwa na sifa za infrared, Wi-Fi na kudhibitiwa kwa kugusa skrini, kifaa hiki kinatazamiwa kuchukua nafasi ya magari ya kupeperusha habari almaarufu Outside Broadcasting yanayotumiwa na kampuni nyingi za matangazo ya runinga.

“Inakuwezesha kurekodi matukio kwa mbashara popote ulipo na video hizi hutumwa moja kwa moja hadi studio ambapo watazamaji wa televisheni wanaweza kuona kwa runinga zao nyumbani,” anaeleza Bw Gabat.

Kufanya hivi, mhudumu anafaa kuiunganisha kwa intaneti kisha kuchukua anwani yake na kuituma kwa studio ambapo mawimbi yake huleta video kama ilivyo nyanjani.

Inamwezesha mtumizi kurekodi video za mbashara na kupakia moja kwa moja kwenye mtandao wa YouTube.

“Video hurekodiwa kwa mfumo wa h.265 bna kupakiwa kwa YouTube kimbashara. Kwa watazamaji wa mitandaoni kuipakua video hii, wanahitaji kupata ruhusa ya aliyeipakia. Imelindwa dhidi ya watu wanaopenda kupakua video za watu kisha kuzitumia kwa manufaa yao ya kifedha.,” anafafanua.

Naye meneja wa biashara endelevu wa Canon Bw Ameur Allag anaonyesha mashine ya kupiga chapa ya kidijitali ambayo anasema ina diski tepetevu (hard disk) isiyoweza kudukuliwa.

“Kwa kuwa wezi wa mashine hizi wamezoea kwena kufuta kila kitu kwenye diski, diski ya mashine hii haiwezi kudukuliwa kamwe. Inatumia teknolojia ya kisasa yakulinda data kwenye diski,” anasema.

Unaweza kuchpisha stakabadhi na nakala ukiwa popote duniani huku data yako ikilindwa kwa nywila katika mtandao wake. Pia unaweza kuchapisha kwa kutumia simu yako kupitia kwa vifushi vya data ya intaneti au Wi-Fi.

Bw Kauangal alisema kwamba kampuni hiyo inajizatiti kuunganisha teknolojia za matangazo ya habari, uundaji wa filamu na upigaji picha kuifaa jamii kwa kurahisisha mambo.

“Ni mara ya kwanza kushuhudia suluhu za kunasa picha safi za ragi kwenye giza. Bila teknolojia, hili halingewezekana,” akasema.