Habari Mseto

Kamishna awaonya wakazi wa Mombasa wanaokiuka masharti ya kuzuia kuenea kwa Covid-19

November 4th, 2020 1 min read

Na WINNIE ATIENO

KAMISHNA wa Kaunti ya Mombasa Gilbert Kitiyo amesema maafisa wa polisi wataendelea kushika doria eneo hilo ili kuhakikisha wakazi wote wanafuata kanuni za kukabiliana na virusi vya corona.

Bw Kitiyo alisema maafisa wa polisi wataendelea kufanya misako ili wakazi wote wavae barakoa, waoshe mikono na hata kutosongamana.

“Tutaendelea kufanya misako kila kuchao kwa sababu idadi ya maambukizi imeongezeka. Isitoshe, hospitali zote hasa katika vitengo vya huduma za dharura, zimejaa na hatutaki watu wengi zaidi wapate maradhi ya Covid-19 na watupatie presha,” alisema Bw Kitiyo.

Kamishna huyo alisema magari ya umma na mabasi ya masafa marefu watapewa uhamasisho ili waendelee kufuata kanuni.

“Hata hivyo ninafurahi wkmaba magari ya umma hasa matatu na mabari wanafuata kanuni za kudhibiti maambukizi kwa asilimia 99, wanahakikisha abiria wanavaa barokoa, wanatumia sanitizana hawasongamani. Lakini ubaya ni kwamba wengine wanavalia barakoa kwa shingo,” alisema Bw Kitiyo aliposimamia msako huko Bonje.

Alisema watu 94 wameaga dunia eneo hilo kwa sababu ya ugonjwa huo huku wengine zaidi ya 3,000 wakiambukizwa virusi hivyo.

“Hivyo vifo vinashtua sana hivyo ni muhimu tuendelee kujikinga,” alisisitiza.