Habari Mseto

Kamishna mkuu KRA awaonywa wanaokwepa kulipa ushuru

August 28th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

UFAGIO wa wanaokwepa kulipa ushuru hauna ubaguzi wala mapendeleo, amesema Kamishna Mkuu mpya wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) James Gathii Mburu.

Kulingana na Kamishna huyu, mjeledi wake hautasaza miamba wakubwa na wenye ushawishi mkuu serikalini, wanaotumia raslimali ya umma kujinufaisha.

Kauli ya Bw Mburu imejiri wakati ambapo hali ya wasiwasi imetanda katika afisi za KRA, baadhi ya maafisa wakuu na wale wadogo katika mamlaka hiyo wakiendelea kuchunguzwa kwa tuhuma za kusaidia wafanyabiashara kuhepa kulipa kodi.

Kamishna huyo Jumanne alisema uchunguzi unaoendelea ni wa ndani na nje ya KRA unaolenga waliokwepa kulipa ushuru na waliosaidia katika kutendeka uhalifu huo.

“Hatuchagui yeyote. Tukinasa waliokosa kulipa kodi, tutaandama waliosaidia kukwepa. Washirika, adhabu i njiani yaja,” alionya.

Alisema idara ya uhalifu wa jinai, DCI na afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma DPP, ni huru na kwamba taasisi hizo zinafahamishwa na umma sakata zinazochezwa katika KRA. “Iwapo hujafanya hatia yoyote, sioni haja ya kuwa na wasiwasi, DCI na DPP wanafanya kazi yao,” akasema.

Onyo lake pia linajiri siku kadhaa baada ya mkurugenzi mkuu wa kiwanda cha kutengenezea vileo cha Keroche mjini Naivasha, Tabitha Karanja na mumewe John Karanja, kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa madai ya kukwepa kulipa kodi. Wawili hao wanasemekana kukwepa kulika kodi ya Sh14.4 nilioni, tangu mwaka 2015 – 2019.

Mnamo Jumanne, Kamishna Mburu alisema takribani kiasi cha Sh250 bilioni, ushuru, ndicho kinakisiwa kukwepwa kulipwa.

Alisema baadhi ya kampuni na mashirika yamekuwa yakitoza wafanyakazi ushuru, pamoja na kutoa huduma kwa gharama ya mlipa ushuru, bila kulipa kodi yoyote kwa serikali.

Pia, alisema baadhi ya wakandarasi katika serikali kuu na serikali za kaunti, wamekuwa wakihepa kulipa ushuru.

“Anayefanya hivyo hana tofauti yeyote na mwizi au mhalifu, anapaswa kushtakiwa kortini,” akasema.

Akaongeza: “Ikiwa mfanyakazi anayepokea mshahara wa Sh20,000 kwa mwezi analipa ushuru, kwa nini si wanaoingiza mabilioni ya pesa?”

Baadhi wajitokeza

Hata hivyo, Bw Mburu alisema wengi wa wafanyabiashara wamejitokeza na kuahidi kulipa kodi.

“Waliojitokeza tumekubaliana mikakati ya kulipa. Ukijitokeza, tutakusaidia namna ya kulipa polepole,” akaeleza Kamishna huyo.

Mburu alisema kila Mkenya akikubali kulipa ushuru, serikali ina uwezo kufanya maendeleo bila mikopo. Alisema anajua mahali pesa ziliko nchini, na kwamba Kenya ni taifa lenye raslimali ya kutosha kuiwezesha kuendesha gange zake na maendeleo bila madeni.

“Sote tukilipa ushuru tunavyofaa, hatuenda nje kukopa, niamini. Tusipolipa ushuru tutaendelea kuwa na madeni,” alisema. Kufikia sasa, taifa hili linakisiwa kuwa na deni zaidi ya Sh4 trilioni.