Habari Mseto

Kamishna wa Machakos aamuru polisi wawakabili wanyakuzi wa vipande vya ardhi waliojihami Athi River

December 20th, 2020 1 min read

Na SAMMY KIMATU

SERIKALI imeamuru maafisa wa polisi katika Kaunti ya Machakos wachunguze na washughulikie ipasavyo watu wanaoshukiwa kuwa na silaha na kuwatisha wamiliki wa ardhi.

Kufuatia madai hayo, kamishna wa kaunti ya Machakos, Bw Fredrick Ndunga aliongoza maafisa wakuu wa kamati ya usalama hadi Ngelani Settlement Scheme Block One katika kaunti ndogo ya Athi River kuliko na ardhi ya kuzozaniwa.

“Niliongoza kamati ya usalama ya kaunti na washiriki wangu wote wa kamati ya usalama tarafani kupata ukweli baada ya mzozo mkali wa ardhi hapa Ngelani Settlement Scheme Block one,” Bw Ndunga alisema.

Alifafanua kuwa mmiliki wa ardhi halisi ni kanisa la Deliverance. Hata hivyo, ardhi hiyo inamezewa mate na watu wengine wanaomiliki silaha na kutaka kunyakua ardhi ya wenyewe.

Aliongeza zaidi kuwa ardhi ilinunuliwa na kanisa na baadaye ikagawanywa kwa washiriki wake. Alitangaza kwamba wanyakuzi wote waachane kabisa na ardhi hiyo na akaamuru polisi washukiwa wowote wa unyakuzi wa ardhi watakaokanyanga ndani ya ardhi hiyo wakabiliwe vilivyo kwa mujibu wa sheria.

Kando na hayo, Bw Ndunga alisema baada ya mashauriano na uchunguzi kukamilika, kanisa lilitoa hati halisi kama uthibitisho wa umiliki wa ardhi hiyo yenye mzozo.

“Nimetoa maagizo kwa polisi washughulikie washukiwa wote wa kuvamia ardhi za wenyewe bila huruma,’’ akanena.

Vilevile, alishauri wakazi wa Machakos wafanye bidii ipasavyo kwa kufanya upekuzi na kushughulikia maswala ya ardhi kutoka kwa ofisi za serikali ili kuepuka kulaghaiwa na matapeli,” Bw Ndunga alisema.

Kadhalika, Bw Ndunga aliwahakikishia wakaazi wa Machakos kwamba atazunguka kote katika kaunti kupata ukweli kutoka kwenye maswala ya ardhi zozote zinazozozaniwa. Hatimaye, alihahidi kutokomeza wote wanaowatapeli watu mamilioni ya pesa katika biashara ‘chafu’ za kuuza na kununua mashamba kwa njia za mikato zilizo kinyume cha sheria.