Kamket alala seli tena Lempurkel akijitetea

Kamket alala seli tena Lempurkel akijitetea

Na WAANDISHI WETU

MBUNGE wa Tiaty, Bw William Kasait Kamket aliyekamatwa Jumatano kuhusiana na mashambulio ya ujangili Kaunti ya Laikipia, alilala seli kwa siku ya pili huku aliyekuwa mbunge wa Laikipia Kaskazini Mathew Lempurkel akishtakiwa kwa kutoa matamshi ya uchochezi.

Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Nakuru Lilian Arika aliagiza Bw Kamket azuiliwe katika kituo cha polisi hadi leo Ijumaa atakapotoa uamuzi kuhusu ombi la polisi wanaotaka wamzuilie kwa siku 14 kukamilisha uchunguzi.

Katika Mahakama ya Milimani, Nairobi, Bw Lempurkel alikanusha mashtaka ya kuchochea chuki za kijamii Kaunti ya Laikipia na akaachiliwa kwa dhamana ya Sh150,000 pesa taslimu.

Maafisa wa uchunguzi wa jinai waliomba waruhusiwe kumzuilia Bw Kamket kukamilisha uchunguzi kuhusu kuhusika kwake katika mashambulio Kaunti ya Laikipia ambapo watu zaidi ya 10 wameauwa na wengine wengi kutoroka makwao.

Mbunge huyo alikamatwa Jumatano alasiri akiwa nyumbani kwake Baringo na kusafirishwa hadi Nakuru kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Kaptembwo.

Polisi waliambia Mahakama kwamba mbunge huyo anashukiwa anahusika kupanga na kuchochea wafugaji kuvamia na kushambulia jamii zinazoishi Ol Moran, Laikipia.

Mwendesha mashtaka wa serikali Alloys Kemo aliambia mahakama kwamba polisi wanamchunguza mbunge huyo kwa mauaji, wizi wa mabavu, wizi wa mifugo, uharibifu wa mali na kuchochea ghasia.

Walisema jinsi mashambulio hayo yalivyotekelezwa kunaonyesha yalikuwa yamepangwa na washukiwa kadhaa akiwemo Bw Kamket.

Hata hivyo, wakili wa mbunge huyo Bw Kipkoech Ngetich alidai ombi la polisi halikuwa na msingi wa kisheria.

Bw Ngetich alilaumu polisi kwa kumkamata mbunge huyo bila ushahidi akisema wanamtumia kuepuka lawama kufuatia kudorora kwa usalama Laikipia.

Polisi waliambia Mahakama kwamba katika uchunguzi wao wanataka kuandikisha taarifa kutoka kwa mashahidi miongoni mwa masuala mengine.

Bw Lempurkel alikanusha shtaka la kuchochea chuki.

Shtaka lilisema kwamba alitenda kosa hilo kati ya Julai 11 na Julai 17 wakati wa mahojiano kwenye kituo cha Televisheni cha jamii ya Maa.

Upande wa mashtaka ulieleza Hakimu Mkazi Bi Sinkiyian Tobiko kwamba kutokana na matamshi ya kuchochea hisia za chuki ya Bw Lempurkel, vurugu zimezuka Laikipia ambapo watu kadhaa wameuawa, mifugo kuibwa, uvamizi wa mashamba ya kibinafsi na watu kuhama makwao.

Kiongozi wa mashtaka Bw Abel Omariba hakupinga mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana.Mawakili Thomas Kajwang, Harun Ndubi na Saitabau ole Kanchory walipinga matamshi ya upande wa mashtaka na kusema suala la mashamba katika eneo la Laikipia ni miongoni mwa dhuluma za kihistoria zinazopasa kujadiliwa na pande zote kwa njia ya amani ili kupata suluhu.

“Suala la umiliki wa mashamba ambalo lilizugumziwa na Bw Lempurkel wakati wa mahojiano katika kituo cha Televisheni cha Maa ni mojawapo ya dhuluma za kihistoria zinazopaswa kujadiliwa bila kuhatarisha haki za wakazi wa maeneo husika,” alisema Bw Kajwang.

Katika uamuzi wake, Bi Tobiko alisema kesi inayomkabili mshtakiwa iko na umuhimu mkubwa kwa umma.

Kesi hiyo itatajwa Septemba 22, 2021 kwa maagizo zaidi.

You can share this post!

WASONGA: Serikali itatue changamoto zinazokumba mtaala mpya

Makala ya spoti- Bandari FC