Habari Mseto

Kamket amuonya Ruto kwa kuhujumu mswada wake

April 17th, 2018 1 min read

Na FLORAH KOECH

MBUNGE wa Tiaty William Kamket Jumanne alimkashifu Naibu Rais William Ruto kwa kuhujumu mswada wake wa kubadilisha katiba ili kubuni wadhifa wa waziri mkuu.

Bw Kamket alisema Bw Ruto anaongoza kundi fulani ndani ya chama cha Jubilee ili kupinga vikali mswada huo ambao anasema unalenga kuhusisha jamii zote katika uongozi wa nchi.

“Watu fulani katika Jubilee wanahisi kuwa mswada huu utawanyima nafasi ya kuwa rais mwenye mamlaka makuu. Ningetaka kuwaonya kuwa hata Raila (Odinga) aliamini sana kuwa rais lakini hajakuwa,”alisema Bw Kamket.

Mbunge huyo ambaye alichaguliwa kupitia tiketi ya chama cha Kanu alisema ni mapema sana kwa wanaopinga mswada huo kuogopa kukosa mamlaka.

“Sielewi kwa nini mswada huu unatia baadhi ya watu tumbo joto na hata hawajui nani atamridhi Rais Uhuru Kenyatta,” alishangaa Kamket.

Alisema anataka kuleta urais katika Kaunti ya Baringo akiongeza kuwa kinyang’anyiro cha 2022 ni kati ya farasi wawili, Seneta wa Baringo Gideon Moi na Naibu Rais William Ruto.

“Safari ya Ikulu imeanza na sharti watu fulani wajitayarishe kwa kipindi kigumu cha kisiasa,” alisema.

Akiongea katika hafla ya harambee eneo la Chepkalacha, wadi ya Tangulbei aliweka wazi kuwa mkutano kati ya Raila Odinga na Rais mstaafu Daniel Moi nyumbani kwake Kabarak ulikuwa kuhusu siasa za 2022.

Mswada wa Bw Kamket unalenga kubadilisha mfumo wa uongozi nchini kwa kupatia bunge mamlaka ya kuchagua rais kwa muhula mmoja.

Mswada huo pia unatoa nafasi ya waziri mkuu kama mkuu wa serikali na manaibu wake na kuondoa wadhifa wa naibu rais.