Habari Mseto

Kampeni ya kuwabamba wazee wanaooa wasichana matineja yaanza

June 21st, 2018 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

IDARA ya usalama ya kaunti ya Lamu imezindua kampeni kabambe ya kuwasaka na kuwakamata wazee wanaowaoa wasichana wa umri mdogo eneo hilo.

Kampeni hiyo pia inalenga kuwanasa wahusika wa ubakaji, washukiwa wa ulawiti wa watoto na wazazi wanaoendeleza ndoa za mapema kwa wasichana wao badala ya kuwahimiza kuzingatia masomo.

Akizungumza na wanahabari ofisini mwake Jumanne, Kamanda Mkuu wa Polisi wa Kaunti ya Lamu, Muchangi Kioi, alitaja kukithiri kwa visa hivyo hasa kwenye maeneo ya Hindi na Mokowe.

Bw Kioi alifichua kuwa zaidi ya watoto saba wamebakwa kwenye vijiji vya Hindi na Mokowe mwezi huu wa Juni pekee ilhali makumi ya wasichana wakiwa wameozwa na wazazi wao.

Alisema operesheni waliyozindua itaangazia sana maeneo hayo mawili.

Alisema inashangaza kwamba baadhi ya wazazi kwenye maeneo hayo wamekuwa mstari wa mbele kuficha ubakaji na ulawiti wa watoto wao badala ya kuripoti visa hivyo kwa polisi ili hatua mwafaka zichukuliwe dhidi ya wahalifu.

Badala yake, wazazi wamekuwa wakishirikiana kisiri na wabakaji, walawiti na hata wale wanaotunga mimba wasichana wa shule ili wasifikiwe na mkono wa sheria.

Kamanda huyo wa polisi alionya vikali wazazi wa namna hiyo kwamba wakipatikana pia watakamatwa na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria.

Alizitaka jamii za Lamu kuheshimu haki za watoto na kuwahimiza wakazi kusomesha wasichana wao ili kujinasua kutoka kwa umaskini uliokithiri.

“Kuna unajisi na ulawiti unaofanywa dhidi ya watoto wadogo hasa eneo la Hindi na Mokowe. Tayari tumerekodi visa zaidi ya saba vya watoto kubakwa na kulawitiwa eneo la Hindi. Wazazi kwenye maeneo hayo pia wamekuwa wakiendeleza itikadi ya kuwaoza mabinti zao wa umri mdogo kwa wazee.

Tumeanzisha kampeni inayolenga kuwakamata wazee wanaooa wasichana wa shule, wazazi wanaooza wasichana wao, wabakaji na wale wanaoendeleza ulawiti wa watoto kote Lamu. Kampeni yenyewe hasa tutaielekeza zaidi Hindi na Mokowe ambapo visa hivyo vimekithiri,” akasema Bw Kioi.

Aliomba mashirika yasiyo ya kiserikali na yale yanayohusika na masuala ya kijamii kuendeleza hamasa kwa wakazi hasa kwenye miji ambayo visa vya ndoa za mapema, ubakaji, ulawiti na mimba za mapema vimekithiri Lamu.

Mnamo Aprili mwaka huu, Shirika la World Vision eneo hilo lilifichua kuwa wasichana wapatao 25 tayri walikuwa wamenajisiwa na wazazi wao kwenye divisheni ya Hindi.

Shirika hilo pia liliorodhesha ndoa za mapema kuwa kizingiti kikuu katika kuendelezwa kwa elimu ya mtoto msichana eneo hilo