Habari Mseto

Kampeni yaja magavana kusisitizia raia umuhimu wa barakoa

November 20th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

BARAZA la Magavana (CoG) linapanga kuzindua kampeni ya kuwahimiza wananchi kuvalia barakoa nyakati zote kabla ya kuhudumiwa katika afisi za serikali zote 47 za kaunti.

Kwenye kikao na wanahabari katika makao makuu ya baraza hilo, Jumba la Delta, Westlands, Nairobi, mwenyekiti wa baraza hilo Wycliffe Oparanya amesema Ijumaa kampeni hiyo inalenga kupiga jeki msimamo wa Serikali Kuu kwamba wajibu wa mtu binafsi ni njia bora ya kudhibiti kuenea kwa Covid-19.

Kauli mbiu ya kampeni hiyo ni “Bila Maski, Hakuna Huduma.”

Hata hivyo Bw Oparanya hakusema ni lini kampeni hiyo inayojulikana kwa kimombo kama “No Mask, No Service”, itaanza kote nchini.

“Kampeni hii itaendeshwa kwa kutumia njia salama na bora za kupitisha ujumbe, zikiwemo redio zinazopeperusha matangazo kwa lugha za kienyeji na mbinu nyinginezo za mawasiliano katika ngazi ya kaunti,” akawaambia wanahabari.

Vile vile, Bw Oparanya alisema serikali za kaunti zinafanya kazi kwa ushirikiano na makamishna wa kaunti, chini ya mwavuli wa Kamati za Kukabiliana na Janga la Covid-19 (CERC).

Hatua za pamoja

Ushirikiano huo, akasema, unalenga kuhakikisha kufanikisha uzinduzi wa hatua za pamoja za kuhakikisha kuwa masharti ya kudhibiti msambao wa corona zinatekelezwa.

Na kama hatua ya kuzuia maambukizi miongoni mwa wahudumu wa afya, Oparanya alisema baraza lake litajizatiti kuhakikisha kuwa wahudumu hao wanapata vifaa kinga (PPEs) vilivyoidhinishwa na Shirika la Kuthibitisha Ubora wa Bidhaa Nchini (KEBs).

“Ili kufanikisha hili, kaunti zinashirikiana kwa karibu na Wizara ya Afya kuhakikisha zinanunua PPEs zenye ubora wa hali ya juu kutoka kwa Mamlaka ya Usambazaji Dawa na Vifaa vya Kimatibabu Nchini (KEMSA),” akasema Bw Oparanya ambaye ni Gavana wa Kakamega.

Wahudumu wa afya wametisha kugoma ikiwa serikali kuu na zile za kaunti hazitahakikisha kuwa wanapewa PPEs zenye ubora wa juu ili kujikinga, miongoni mwa sababu nyinginezo.

Hii ni kufuatia vifo vya madaktari na wahudumu wengine wa afya baada ya kuambukizwa virusi vya corona.

Kenya imeandikisha idadi ya juu ya maambukizi tangu mwezi jana ambapo kufukia Ijumaa, Novemba 20, 2020, idadi jumla ya maambukizi ilikuwa imetimu 75, 190 huku idadi ya waliofariki ikifikia 1, 349. Hii ni baada ya watu 19 zaidi kuthibitishwa kufariki kutokana na corona Ijumaa.

Mnamo Alhamisi, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilizindua kampeni kwa jina “Mask Up, Not Down” inayolenga kuwahimiza watu kuvalia barakao ipasavyo ili kujikinga na maambukizi.

Kampeni hiyo inalenga kuwafikia zaidi ya vijana 40 milioni kote Afrika kupitia mitandao ya kijamii miongoni mwa njia nyinginezo za mawasiliano.