Habari Mseto

Kampuni kadha za kamari zakabwa koo nchini Kenya

July 11th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imefutilia mbali leseni za kuhudumu za kampuni 27 za kamati zinazohudumu nchini kwa kufeli kuthibitisha kuwa huwa zinalipa ushuru inayohitajika.

Kufuatia hatua hiyo Bodi ya Kusimamia sekta ya Kamari (BCB) Jumatano iliamuru kampuni zote za kutoa huduma za kutuma na kupokea pesa kuondoa nambari za malipo (Pay Bill Numbers) za kampuni husika.

“Tungependa kufahamisha umma kwamba leseni za kampuni za Kamari zifuatazo hazikutolewa upya kwa sababu zilikosa kutimiza masharti yaliyowekwa na matokeo ya uchunguzi unaoendelea kubaini ikiwa zinaweza kuendelea na shughuli zao. Kwa hivyo, tunashauri msimamishe nambari zao za malipo hadi mtakapopata ushauri kutoka kwa bodi hii,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa BCB Liti Wambua kwenye taarifa iliyotumwa kwa kampuni za kutoka huduma za kutuma na kupokea fedha.

Kampuni za huduma hizo ni Safaricom, Airtel na Telkom Kenya.

Nazo kampuni ambazo ziliathirika ni zifuatazo:

1. SportPesa

2. Betin

3. Betway

4. Betpawa

5. Elitebet

6 PremierBet

7. Lucky2u

8. 1xBet

9. MozzartBet

10. Dafabet

11. World Sports Betting

12. Atari Gaming

13. Palms Bet

14. Betboss

15. Kick-Off

16. Millionaire Sports Bet

17 Cheza Cash

18 Betyetu

19. Bungabet

20. Cysabet

21. Saharabet

22. Easibet

23.Easleighbet

24. Sportybet

25. AGB lottery and gaming

26. Atari 27.

27. Kickoff

Bw Wambua alisema kampuni hizo zitaruhusiwa tu kuendesha shughuli zao humu nchini baada ya uchunguzi unaoendelea kubaini kuwa zimekuwa zikilipa ushuru kulingana na sheria iliyowekwa.

Katika Bajeti aliyoisoma bungeni mwezi Juni, Waziri wa Fedha Henry Rotich alipendekeza ushuru wa asilimia 10 kwa kiwango chochote cha fedha ambazo mtu atatumia kucheza kamari.

Madhara ya kijamii

Alisema hiyo ni mojawapo ya hatua za kudhibiti uraibu huo ambao umeteka mawazo na nyonyo za Wakenya – hasa vijana – hali inayosababisha madhara mengi ya kijamii.

Bw Rotich alisema ipo haja kwa serikali kuwalinda vijana kutokana na madhara yanatokana na utamaduni huo wa uchezaji Kamari.

“Uchezaji kamari umeenea zaidi katika jamii zetu kiasi kwamba unasababisha madhara makubwa; hasa kwa vijana na watu wengine wasio na mapato ya juu. Ushuru huu wa asilimia 10 ni mojawapo kati ya hatua kadha ambazo serikali inapanga kuchukua kupunguza uraibu huu,” akasema Bw Rotich.

Kando na hatua hiyo, Sheria ya Fedha ya mwaka wa 2018 inawaadhibu waraibu wa mchezo wa kamari kwa kuwatoza ushuru wa asilimia 35.

Asilimia 20 ya fedha hizo hutolewa kutoka kwa kiasi cha fedha ambazo mtu ameshinda huku asilimia 15 zilizosalia zikilipwa na kwa Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) na kampuni husika za kamari.