Habari Mseto

'Kampuni ya Delmonte bado ni tegemeo kwa wafanyakazi Thika'

June 30th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KULINGANA na mpangilio ulioko muda wa ardhi ya kampuni ya Delmonte Ltd mjini Thika kutwaliwa na serikali baada ya miaka 99, ni mwaka wa 2022.

Hivi majuzi mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alipeleka mswada bungeni akiiomba serikali iongeze muda zaida kwa kampuni hiyo kuendelea na biashara mjini Thika.

Alimsihi Rais Uhuru Kenyatta aingilie kati ili kuona ya kwamba kampuni hiyo inaongezewa muda zaidi ili iendelee na shughuli zake za kutengeneza sharubati ya mananasi.

“Iwapo kampuni hiyo itafunga shughuli na kuhamia nchi zingine za nje, wafanyakazi zaidi ya 6,500 wa kudumu na vibarua wapatao 28,000 watapoteza ajira mara moja,” alisema Bw Wainaina.

Ilidaiwa iwapo kampuni hiyo itahamisha shughuli zake kutoka nchini Kenya huenda ikapoteza takribani Sh10 bilioni kwa mwaka.

Hata hivyo, ardhi ya kampuni hiyo imekuwa na mvutano kati ya kaunti mbili ya Kiambu na Murang’a ambazo zimeenea sehemu hizo mbili.

Lakini mwaka wa 2019, tume ya ardhi ya NLC, ilizuru ardhi hiyo ya Delmonte ili kutathmini jinsi mambo yalivyo.

Baadaye tume hiyo alitoa amri kuwa ardhi ya ekari 7,400 ifanyiwe ukaguzi upya ili kutoka na hali kamili ya mambo.

Wakati huo pia mbunge huyo alipendekeza Wizara ya Ardhi ifanye mpango kuwaleta maafisa wa ardhi mjini Thika miezi michache ili kutatua shida nyingi za ardhi zinazokumba wakazi wa eneo hili.

Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa wakongwe wengi wamepoteza vipande vyao vya ardhi kwa matapeli huku wakipokea vyeti ghushi.

Mpango huo wa kliniki uliendeshwa mjini Ruiru, na kufaulu mwaka 2019 ambapo shida nyingi za ardhi zilitatuliwa.

Wakazi wa Thika wanangoja maafisa hao wa ardhi wafike mjini Thika na kutatua shida nyingi zinazowakumba eneo hilo.