Habari Mseto

Kampuni ya India yaruhusiwa kuuza mbegu za GMO

August 13th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Serikali imetoa idhini kwa kampuni ya India kununua mbegu za pamba zilizotengenezwa kiteknolojia (GMO) kuwauzia wakulima wa humu nchini.

Kupitia kwa kampuni ya Maharashtra Hybrid Seeds Co (Mahyco), wakulima wa pamba ambao wangependa kujaribu pamba aina ya GMO watakuwa na uwezo wa kuipata.

Lakini kwanza pamba hiyo inafanyiwa majaribio katika maeneo kadhaa nchini kabla ya wakulima kukubaliwa kuipanda.

Kampuni hiyo itasambaza mbegu hiyo kwa niaba ya Monsanto. Hii ni baada ya Mamlaka ya Kitaifa Kusimamia Mazingira (NEMA) kutoa idhini ya kufanywa kwa majaribio hayo nchini.

Hiyo ni hatua inayoonyesha kuwa serikali huenda ikawa tayari kuondoa marufuku ya miaka sita ya uagizaji wa GMO nchini.

Huenda mwaka ujao wakulima wakakubaliwa kuanza kukuza pamba ya GMO kote nchini baada ya majaribio hayo.

Majaribio hayo yanafanyiwa Mwea, Bura Tana, Katumani, Kampi ya mawe (Makueni) na Perkerra katika Kaunti ya Baringo.