Habari Mseto

Kampuni ya Kenya yatia fora Tanzania kwenye KPMG Top 100

November 15th, 2018 1 min read

Na FAUSTINE NGILA

KAMPUNI moja ya Kenya imeorodheshwa miongoni mwa kampuni bora zaidi katika mashindano ya Kampuni Bora 100 yaliyoandaliwa na KPMG nchini Tanzania, baada ya kutajwa katika kampuni 50 za kwanza kati ya kampuni zote za taifa hilo.

Kampuni ya Vehicle and Equipment Leasing Limited (VAELL) ilipiku kampuni 55 ambazo zilishiriki mashindano hayo na kuorodheshwa nambari 45.

Kampuni za Kibo Palace Hotel and Resort, Xpres Rent A Car na Brett & Beileys (T) Limited zilichukua nafasi za kwanza tatu.

Kampuni hiyo ambayo makao yake makuu yako Kenya na pia ina matawi mengine 18 barani Afrika mbeleni imeshinda mashindano sawia Kenya, Uganda na Afrika Kusini na tuzo hii ilikuwa ya pili mwaka huu.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, imeshinda tuzo 14. Mara yake ya kwanza kuorodheshwa katika mashindano ya KPMG ilikuwa 2012.

Mnamo 2012, Vaell Kenya iliorodheshwa nambari mbili katika utafiti huo wa kampuni 100 bora ambao huendeshwa na KPMG na kampuni ya Nation Media Group, ambao hutafiti kampuni zinazokuwa kwa kasi zaidi nchini.

Kampuni hiyo hufanya kazi ya kukodesha na kusimamia magari na vifaa vya mashine kwa kampuni za kufanya kazi za uhamishaji wa mali.

Akipokea zawadi hiyo, meneja wa mauzo Vaell tawi la Tanzania Julie William Kibera alisifu usimamizi mwema na utaalamu kuwa umesababisha kampuni hiyo kutuzwa kote.

“Matawi mengine yetu yamekuwa yakipokea tuzo kutokana na uongozi sokoni. Hii ni kwa ajili ya kujitolea na utaalam wa wafanyakazi wetu,” akasema.

Aidha, kampuni hiyo imesifiwa kuwa na akaunti zilizokaguliwa vyema, baadhi ya sababu zilizofanya mwaka huu kutajwa kampuni bora zaidi Afrika Mashariki kwa utoaji wa huduma na Baraza la Biashara ya Afrika Mashariki huko Tanzania.