Habari Mseto

Kampuni ya mikopo yajitenga na wizi wa bodaboda

June 5th, 2024 1 min read

NA WACHIRA MWANGI

KAMPUNI ya kutoa mikopo ya kununua pikipiki, imejiondolea lawama kuhusu madai kwamba baadhi ya kampuni aina hiyo nchini huhusika katika wizi wa pikipiki za wahudumu wa bodaboda.

Meneja wa Kamuni ya Watu Credit nchini, Bw Erick Mwassame, alisema hakuna vile wanaweza kuhusishwa na madai hayo ilhali pikipiki inapopotea kabla malipo yakamilishwe, wao hupata hasara.

“Hakuna njia yoyote Watu Credit inaweza kuhusika katika wizi wa pikipiki wakati tunapoteza mali na wateja wetu. Hali ni ya kutisha na tunafanya kazi na vitengo vya usalama kote nchini kushughulikia suala hili,” alisema Bw Mwassame.

Kampuni hiyo imeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa matukio ya wizi wa pikipiki na vifo vya waendeshaji wa pikipiki kote nchini.

Bw Mwassame alibaini kuwa kumekuwa na zaidi ya kesi 1,100 za wizi huku Kaunti ya Mombasa pekee ikiwa na matukio 202 tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Bw Mwassame alisisitiza kuwa Watu Credit imewekeza sana katika miundombinu imara ili kudhibiti masuala ya usalama kwa wateja wao.

“Tunaendesha kituo cha simu za dharura kushughulikia matatizo ya wateja na tumefanikiwa kurejesha asilimia 54 ya mali zote zilizoibiwa. Eneo la pwani limeona ongezeko kubwa la wizi wa pikipiki na mauaji.

“Tunajihusisha kikamilifu na jamii za bodaboda na viongozi wao ili kushughulikia masuala haya ya usalama,” alieleza Bw Mwassame.

Kampuni hiyo pia inashirikiana na usimamizi wa usalama wa kaunti kukomesha wizi huu unaokithiri.

Kupotea kwa pikipiki kumeathiri moja kwa moja biashara ya Watu Credit, na kusababisha hasara ya mali.

Gavana wa Kaunti ya Taita Taveta, Andrew Mwadime, hivi majuzi alitangaza marufuku ya muda kwa mashirika mawili ya mikopo ya bodaboda kufuatia mauaji na wizi wa waendeshaji bodaboda wanane katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita katika kaunti hiyo.