Kampuni ya Mumias mbioni kurejelea usagaji wa miwa

Kampuni ya Mumias mbioni kurejelea usagaji wa miwa

Na SHABAN MAKOKHA

KAMPUNI ya Sukari ya Mumias imeanza shughuli za kuhesabu miwa ili kubaini idadi iliyopo, ikilenga kurejelea tena usagaji wa zao hilo.

Ijumaa, mkurugenzi wa kitengo cha masuala ya sheria, Bw Patrick Mutuli, alisema kwamba wamewatuma maafisa maalum nyanjani kubaini idadi ya miwa iliyopo ili warejelee usagaji miwa.

Kampuni hiyo, inayokumbwa na changamoto za kifedha ilisimamisha shughuli hizo mnamo 2018.

Hili ni baada ya wakulima kung’oa zao hilo mashambani mwao, wakiilaumu kampuni kwa kukosa kuwalipa vizuri kwa miwa waliyowasilisha kwake.

Zaidi ya hayo, wakulima walilalamikia kucheleweshewa malipo yao na ada za juu za usafirishaji miwa walizokuwa wakitozwa na kiwanda hicho.

Aidha, walikilaumu kiwanda kwa kuondoa ada za fatalaiza na pembejeo nyingine katika malipo yao licha ya kutopata bidhaa hizo kutoka kwa kampuni.

Hata hivyo, usimamizi wa kiwanda ulivilaumu viwanda vingine kwa kuingilia shughuli zake, hali iliyochangia uhaba mkubwa wa miwa ya kusagwa.

Kampuni hiyo iliyo kubwa zaidi katika eneo la Magharibi, iliwekwa kwenye mnada na Benki ya Kenya Commercial (KCB) mnamo Septemba 2019.

Kulikuwa na matumaini kwamba benki hiyo ingeshirikiana na Wizara ya Fedha kubuni mpango na utaratibu maalum ambao ungeifufua tena na kuisaidia kulipa baadhi ya madeni iliyodaiwa.

Msimamizi mkuu wa mpango huo, Bw Ponangali Rao, aliahidi kukifufua upya kiwanda hicho baada ya mwaka mmoja.

Baada ya mipango hiyo kugonga mwamba, alisema angeegemea uzalishaji wa ethanol ili kumwezesha kupata fedha. Kiwanda hicho kilianza kununua na kuzalisha molasses kutoka viwanda vingine.

Baada ya miezi 15, Bw Rao alisema mipango ya kufufua upya kiwanda hicho ilikuwa ikikumbwa na changamoto.

Wabunge Ayub Savula (Lugari), Benjamin Washiali (Mumias Mashariki) na marehemu Justus Murunga (Matungu) walielezea tashwishi zao kuhusu juhudi alizokuwa akiendeleza Bw Rao, kwani hawakuwa wakiona mabadiliko yoyote tangu achukue uongozi wa kampuni hiyo.

Viongozi hao walitaka kujua faida ambayo kiwanda hicho kilipata kutokana na uuzaji wa ethanol na ikiwa Bw Rao alikuwa akipiga hatua katika kulipa mkopo wa Sh2 bilioni kutoka kwa benki hiyo.

Hata hivyo, Bw Rao amebaki kimya. Inadaiwa alizuru kiwanda hicho mara ya mwisho mnamo Machi 2020.

You can share this post!

ODM iko imara, tayari kutwaa urais – Sifuna

Lille wakomoa Lens na kuweka mkono mmoja kwenye taji la...