Habari Mseto

Kampuni ya Mumias yakana madai kwamba imefilisika

March 18th, 2019 1 min read

Na SHABAN MAKOKHA

WASIMAMIZI wa Kampuni ya Sukari ya Mumias wamekanusha madai ya baadhi ya wanasiasa kutoka Kakamega kwamba kampuni hiyo imefilisika.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Bw Isaac Sheunda alisema licha ya changamoto za kifedha ambazo zimeathiri shughuli zao, kuna asasi ambazo zimejitolea kuwakopesha fedha za kutekeleza mipango yao ya kuifufua.

Akizungumza na wanahabari katika majengo ya kampuni hiyo wiki iliyopita, Bw Sheunda alisema kuwa alikutana na wakopeshaji kupanga jinsi wanaweza kufufua shughuli za kampuni hiyo.

Kampuni ya Mumias inakumbwa na madeni ya mabilioni ya pesa.

“Wakopeshaji ikiwemo serikali wamejitolea kwa dhati kutusaidia kutekeleza mipango yetu ya kufufua Mumias,” akasema.

Alisema licha ya kudaiwa pesa nyingi, hakuna shirika linalowadai ambalo limeonyesha nia ya kutwaa mali za kampuni hiyo kugharimia madeni yake.

Serikali ilitumia zaidi ya Sh3.7b kusaidia kampuni hiyo inayotatizika kifedha.

Aliyekuwa Waziri wa Michezo, Bw Rashid Echesa na Mbunge wa Mumias Mashariki, Bw Benjamin Washiali awali walikuwa wamedai kuwa kampuni hiyo imepangiwa kuwekwa chini ya usimamizi maalumu ili kutatua madeni yake.