Habari za Kitaifa

Kampuni ya simiti yazuiwa kutoa makaa bandarini

January 10th, 2024 2 min read

NA BRIAN OCHARO

SHUGHULI katika kiwanda cha simiti cha Bamburi Cement jijini Mombasa zimo hatarini, baada ya Serikali ya Kaunti ya Mombasa kuzuia kampuni hiyo kusafirisha makaa ya mawe kutoka Bandari ya Mombasa.

Kampuni hiyo huagiza makaa ya mawe kutoka nchi za nje, na kuyatoa bandarini hadi machimbo yake eneo la Kisauni kisha baadaye kutumiwa kama kawi kwa utengenezaji simiti.

Hata hivyo, wiki iliyopita, baadhi ya wakazi wa Mombasa wanaopakana na machimbo hayo, walilalamikia uwezekano wa kuzuka kwa magonjwa walipogundua chembe za makaa hayo hupeperushwa na upepo na kuingia katika nyumba zao.

Naibu Gavana Francis Thoya na maafisa kutoka Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (Nema), walisema rundo kubwa la makaa ya mawe yaliyosagwa ni hatari kuwekwa katika eneo la wazi.

“Eneo hili litasalia kufungwa hadi hatua za kurekebisha zichukuliwe kuzuia vumbi la sumu kuathiri wakazi. Kampuni hairuhusiwi kusafirisha makaa hadi itakapoonyesha jinsi tatizo hili litakavyotatuliwa,” Bw Thoya alisema.

Kampuni hiyo hivi majuzi iliagiza tani 50,000 za makaa ya mawe. Baadhi ya bidhaa hiyo bado haijapakuliwa kutoka kwa meli ambayo imetia nanga katika bandari ya Mombasa.

Wakazi katika kaunti ndogo za Nyali na Kisauni ndio walioathirika zaidi.

Nyumba zao ziko umbali wa kilomita tatu kutoka kwenye machimbo ambapo rundo la makaa ya mawe huwekwa.

“Hakuna shughuli zinazopaswa kuendelea hapa hadi makaa ya mawe yahifadhiwe ipasavyo katika eneo lililofunikwa,” akasema Bw Thoya.

Kaunti hiyo pia imeagiza kampuni zote kuzingatia kanuni za kimazingira kikamilifu.

Kampuni hiyo ilikiri kupokea malalamishi kutoka kwa wakazi wa eneo hilo kuhusu vumbi kutoka kwa kiwanda chake cha Mombasa na kusema kuwa imechukua hatua kushughulikia suala hilo.

Ilisema kuwa ukaguzi wa ndani ulibaini kuwa tukio hilo halijawahi kutokea awali, na mara hii lililsababishwa na upepo mkali ambao ulibeba vumbi hadi mitaani wakati wa kuhifadhi makaa yaliyosalia.

“Tumeongeza unyunyizaji wa maji katika barabara za usafirishaji na maeneo ya kuhifadhi ili kuzuia vumbi kupeperushwa. Tukio hili lilikuwa la kwanza na kwa bahati mbaya lilitokana na upepo mkali ambao haujawahi kuvuma wakati mwingine,” kampuni hiyo ilisema katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Kampuni hiyo imeeleza kuwa inashirikiana na mamlaka husika za kitaifa na kaunti na kushirikiana na jamii kuwahakikishia kuwa hilo ni tukio la pekee lililosababishwa na upepo mkali.

Ilizidi kusema, imekuwa shirika linalowajibika na imekuwa ikifanya kazi kwa miongo kadhaa, na hakuna tukio kama hilo limewahi kutokea hapo awali.

Bamburi Cement ilianza shughuli zake Mombasa katika miaka ya hamsini (1950s) na kufikia sasa imekua hadi kuwa miongoni mwa kampuni kubwa zaidi za utengenezaji simiti ukanda wa Afrika Mashariki.

Hatua hii ya kuzuia makaa ya mawe huenda ikayumbisha ujenzi wa nyumba za bei nafuu ambazo Rais William Ruto anapigia debe.