Habari Mseto

Kampuni ya sukari ya Mumias yawekwa chini ya mrasimu

September 25th, 2019 2 min read

Na BENSON AMADALA na CHARLES WASONGA

MASAIBU ya kampuni ya sukari ya Mumias yaliongezeka Jumanne baada ya Benki ya Kenya Commercial kuteua meneja mrasimu kusimamia shughuli zake.

Benki hiyo iliteua Bw Ponangipalli Venkata Ramana Rao wa kampuni ya ushauri ya Tact Consultancy Services kusimamia shughuli za kampuni hiyo kubwa zaidi nchini.

Hatua hiyo imeshtua usimamizi wa kampuni hiyo na wafanyakazi kwa mshangao mkubwa.

Bw Rao alizuru kiwanda cha kampuni hiyo Jumanne na akawapa wasimamizi stakabadhi kuhusu shughuli za kampuni hiyo katika siku za hivi karibuni.

Mrasimu huyo alikuwa na kaimu mkurugenzi anayesimamia masuala ya wafanyakazi Bw John Shiundu na akampa stakabadhi zinazohusiana na kutwaliwa kwa usimamizi wa kampuni hiyo.

Lakini Seneta wa Kakamega Cleophas Malala alisisitiza kupinga hatua hiyo.

Barua kutoka kwa kampuni ya Tact Consultancy Services inasema hivi: Kulingana na mamlaka niliyopewa kulingana na sheria, Benki ya KCB imemteua Ponangipalli Venkata Ramano Rao wa Tact Consultancy Services, S.L.P 51-00623, Nairobi, Kenya (Mrasimu), kama Meneja Mrasimu wa Kampuni ya Sukari ya Mumias mnamo Septemba 20, 2019.

Hatua hii imefifisha matumaini ya kufaulu kwa mpango unaoendeshwa na serikali ya Kaunti ya Kakamega wa kufufua kampuni hiyo. Kuwekwa kwa kampuni hiyo chini ya usimamizi wa mrasimu pia kutavuruga mipango ya serikali ya kitaifa ya kuikomboa kampuni hiyo.

Katika barua hiyo, meneja huyo mrasimu alisema: “Tafadhali zingatia kuwa wakurugenzi, wenyehisa, wafanyakazi au mtu yeyote, hawaruhusiwi kuendesha shughuli zozote kwa niaba kampuni hiyo bila idhini, kwa maandishi, kutoka kwa mrasimu.”

Taarifa

Usimamizi wa kampuni hiyo imeshauriwa kuwasilisha taarifa kuhusu masuala ya kampuni hiyo kuanzia tarehe ya kuteuliwa kwa mrasimu.

Vilevile, wasimamizi hao wanahitajika kuwasilisha orodha ya mali zote, ikiwemo magari yote na vifaa vinginevyo.

Vilevile, wanahitajika kuwasilisha nakala halisia za vyeti vya umiliki wa ardhi, vyeti vya umiliki wa magari na mali nyinginezo.

Hatua hii inajiri baada ya Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya kuzindia ripoti ya jopokazi aliloteua.

Ripoti hiyo ilizinduliwa wiki tatu zilizopita.

Jopokazi hilo lilijumuisha kundi la maafisa wa serikali ya kaunti ilielezea mikakati ya kufufua kampuni ya Mumias.

Gavana Oparanya alisema serikali yake itashikiza kuteuliwa kwa msimamizi ambaye atazuia kampuni hiyo kuangamia.

Alisema serikali yake itatekeleza yaliyomo katika ripoti hiyo kupitia idara husika katika kampuni hiyo.

Bw Oparanya pia aliahidi kuhakikisha kuwa watu wenye ushawishi waliohusika katika ufujaji wa rasilimali ya kampuni hiyo, wakiwemo mameneja wa zamani na wanasiasa, wanachukuliwa hatua za kisheria.

Kama hatua ya kulinda mali ya kampuni hiyo, serikali ya Kaunti ya Kakamega inapanga kuzima shughuli zozote za uuzaji na ununuzi wa ardhi.

Ripoti hiyo itawasilishwa katika bunge la Kakamega ili ijadiliwe na kupitishwa kabla ya mapendekezo yake kutekelezwa.

Alisema serikali yake itahakikisha walioiba mali za kampuni ya Sukari ya Mumias wanachukuliwa hatua na Idara ya Upeleleza wa Jinai (DCI).

Miongoni mwa mapendekezo katika ripoti ya jopokazi la Bw Oparanya ni kwamba kaunti hiyo itaunga mkono Mswada wa Sukari wa 2019 ambao utawasilishwa bungeni hivi karibuni. Mswada huo unalenga kulinda sekta ya sukari.

“Serikali ya kaunti inalenga, katika bajeti ya ziada ijayo, kuunda hazina ambayo itaimarisha kilimo cha miwa. Sh100,000 zinafaa kutengwa kwa kila ekari kustawisha kilimo hicho katika kila ekari ya kipande cha ardhi ambako kumepandwa miwa,” Bw Oparanya akasema.