Habari Mseto

Kampuni ya Uchina kubuni nafasi 300,000 za ajira

November 6th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Watengenezaji wakubwa zaidi wa hariri (silk) ulimwenguni, Guangdong Silk-Tex Group, wamebuni mpango wa kuzindua kampuni yao nchini.

Hii ni baada ya maafisa wakuu wa kampuni hiyo kukutana na Rais Uhuru Kenyatta Jijini Shanghai, China, alipozuru nchini humo kwa ziara ya maonyesho ya kibiashara.

Kampuni hiyo imepanga kuanzisha operesheni zake eneo la Athi River, Export Processing Zone (EPZ) na kuanzisha shamba la kukuza hariri.

Shamba hilo litakuwa la ekari 8,237 na kubuni nafasi 300,000 za kazi kwa Wakenya kulingana na taarifa kutoka Ikulu.

Wakati huo, shirika la Cherami China-Africa Investment Management lilitangaza azimio lake la kujenga kituo cha kutibu kansa Kenya kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Nairobi.