Kampuni yafuta shoo ya Olomide jijini

Kampuni yafuta shoo ya Olomide jijini

Na HILLARY KIMUYU

KAMPUNI ambayo ilikuwa ikiandaa tamasha la burudani ambalo lingeongozwa na mwanamuziki mashuhuri Koffi Olomide Jumamosi ijayo, imefuta hafla hiyo na kutangaza kuwa walionunua tiketi, watarudishiwa hela zao.

Tamasha hilo kubwa lilifaa kufanyika katika Water Front Mall, mtaani Karen, lakini Afisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Aces and Light, K.K.L Wesley, alisema limefutiliwa mbali na walionunua tiketi watarejeshewa pesa zao.

Koffi ambaye alifurushwa na kurejeshwa kwao Congo kwa lazima na serikali ya Kenya mnamo 2016, baada ya kumpiga mmoja wa wasakataji densi wa kundi lake, ni kati ya wanamuziki ambao muziki wao ni maarufu na umesifiwa sana kote ulimwenguni.

“Kampuni ya Aces and Light imeamua kusitisha maandalizi ya tamasha la muziki ambalo Koffi Olomide angetoa burudani pamoja na bendi yake ya Orchestra International Grand Mopao. Hatua hiyo itahakikisha kuwa tunajiandaa vyema kabla ya kutangaza tarehe mpya,” akasema Bw Wesley.

Baada ya tukio la 2016, Bw Omide aliomba msamaha kwa Wakenya na ulimwengu na serikali nayo ikaondoa marufuku ambayo ilimwekea ya kutokanyaga Kenya.

You can share this post!

Balozi wa zamani ajiunga na siasa

KFS yawahakikishia wakazi huduma za feri zitarejea mwaka...

T L