Habari Mseto

Kampuni yaondoa matatu barabarani wafanyakazi wasiambukizwe corona

March 23rd, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MAGARI ya kubeba abiria ya R.O.G yanayotegemewa sana na wakazi wa Kariobangi South, Nairobi yameondolewa barabarani.

Duru zinasema kampuni ya R.O.G iliagiza Jumapili kuwa wafanyakazi wasifike kazini kuanzia Jumatatu asubuhi wasije wakaambukizwa virusi hatari vya corona vinavoyozidi kutesa ulimwengu.

Magari hayo, ambayo siku ya kawaida hurausha watu mapema asubuhi (saa kumi na moja asubuhi) kwa kupiga honi, hayakusikika ya kipiga kelele hizo.

Mwandishi huyu alipofika katika steji ya Kariobangi South Civil Servants saa nne asubuhi, yanapogeukia magari hayo, alithibitisha hakuna hata gari moja kutoka kampuni hiyo lilikuwa limeonekana.

Kampuni hiyo ina magari yanayohudumu kutoka jumba la Gill House katikati mwa jiji la Nairobi hadi Kariobangi South kupitia Jogoo Road na mtaa wa Buruburu.

Wakazi wengi wamelazimika kutumia magari ya nambari 36 ya kutoka Dandora yanayotamatisha safari zao City Stadium.

Yameongeza nauli kutoka Sh60 hadi Sh80. Wakazi wa Kariobangi South pia wanalazimika kulipa Sh30 kutoka City Stadium hadi jijini. Nauli kati ya Kariobangi South na Gill House kwa kawaida huwa Sh70.

Njia nyingine mbadala ambayo wakazi wa Kariobangi South hutumia kufika jijini ni ile ya barabara ya Juja Road ama Thika Road, ambayo magari yanayohudumu ni nambari 32 ya kutoka Dandora.

Magari haya yaliendelea na shughuli yao kama kawaida. Hata hivyo, wengi wa wakazi wa Kariobangi South huepuka magari ya Dandora kwa sababu nauli yake huwa juu kuliko ile ya magari ya nambari 23 yanayohudumu kati ya jijini na Kariobangi South kupitia Jogoo Road na Buruburu.