Kampuni yashtakiwa kwa kuharibu mti wa Raila

Kampuni yashtakiwa kwa kuharibu mti wa Raila

Na GEORGE ODIWUOR

WANAHARAKATI watatu katika Kaunti ya Homa Bay, wameishtaki kampuni ya kutengeneza vinywaji ya Coca-Cola, kwa dai la kuharibu mti aina ya Mugumo uliopandwa na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Bw Odinga alipanda mti huo katika Uwanja wa Posta, mjini Homa Bay miaka saba iliyopita.

Wanaharakati hao sasa wanaitaka mahakama kuishinikiza kampuni hiyo kupanga jinsi Bw Odinga atarejea mjini humo na kupanda mti mwingine aina hiyo, ambao wenyeji huuita “Bongu.”

Bw Odinga alipanda mti huo mnamo Agosti 2, 2014 alipozuru mji huo kwa hafla ya kisiasa na kuukaribisha rasmi mfumo wa ugatuzi.

Wanachama wa vuguvugu la kisiasa la Bunge la Wenye Nchi, ambalo huendesha shughuli zake eneo hilo, wanaamini mti huo ulikuwa ishara ya kulikomboa eneo la Nyanza kutoka kwa changamoto za kisiasa na kiuchumi.

Mnamo Machi 25, 2017, gari aina ya Pick-up la Coca Cola lilidaiwa kuukanyanga na kuuharibu mti huo lilipokuwa likirudi nyuma.

Wafuasi wa ODM ambao walikuwa wakiunyunyizia maji mti huo kila asubuhi, walishinikiza hatua kali kuchukuliwa dhidi ya dereva aliyekuwa akiliendesha gari hilo pamoja na kampuni aliyofanyia kazi.

Kisa hicho kiliripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Homa Bay.

Inadaiwa kampuni hiyo ilijaribu kuupeleka mti mwingine uliofanana na huo lakini wenyeji haukuwaridhishwa nao.

Uchunguzi uliofanywa na Shirika la Kusimamia Misitu (KFS) mnamo Aprili 2017 ulieleza kwamba gharama ya mti huo ilikuwa Sh68,000.

Mnamo Jumanne, wanaharakati Evance Oloo, Michael Kojo na Walter Opiyo waliwasilisha kesi katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi mjini Migori wakishikilia kuwa chini ya itikadi za jamii zao, mti aina hiyo unapaswa kulindwa sana.

Kampuni ya Coca-Cola, Kisii Bottlers na Almasi Beverages zimeorodheshwa kama washtakiwa.

Baraza la Wazee wa Jamii ya Waluo na Bw Odinga pia wameorodheshwa kama wahusika kwenye kesi hiyo.

Wanaharakati hao walisema kuwa mti huo unapaswa tu kupandwa na Bw Odinga kutokana na ushawishi wake mkubwa katika maisha ya jamii ya eneo hilo.

Walisema huenda mti huo ukakosa kukua ikiwa utapandwa na mtu mwingine mbali na Bw Odinga.

Jaji G. Ongondo alisema kesi hiyo itasikilizwa kuanzia Juni 21, 2021, ambapo wanaharakati hao wanatarajiwa kuwasilisha malalamishi yao.

You can share this post!

Walimu watakaosahihisha KCPE watakuwa katika mazingira...

De Bruyne na Lukaku waongoza Ubelgiji kupepeta Wales katika...