Habari za Kitaifa

Kampuni zaacha mashine za kuchuma majanichai na kurejea kwa vibarua wa mikono

April 12th, 2024 2 min read

Na BARNABAS BII

BAADHI ya kampuni za kuendesha kilimo cha majani-chai katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa zimerejelea uchumaji kwa mikono.

Kampuni hizo zinasema kuwa zimerejelea mtindo huo wa zamani wa uchumaji wa matawi mawili ya juu ya majani-chai, ili kupambana na ushindani mkali katika mnada wa zao na hivyo kuongeza mauzo.

Kampuni hizo zilipoanzisha mtindo wa uchumaji majani chai kwa mashine, viongozi wa kisiasa na wale wa vyama vya wafanyakazi wa mashamba makubwa waliibua malalamishi.

Walisema kuwa mbinu hiyo ni tishio kwa maelfu ya wafanyakazi katika sekta hiyo ya majani-chai.

Mwaka jana, baadhi ya mashine za uchumaji ziliteketezwa na waandamanaji katika maeneo ya kaunti za Bomet na Kericho na kuchangia kukamatwa kwa baadhi ya watu hao.

Lakini sasa kampuni ya Sotik Tea, ambayo kulingana na Chama cha Wafanyakazi wa Mashamba Makubwa Nchini (KPAWU) imeamua kuajiri wafanyakazi 600 zaidi kuchuma majani chai kwa mikono.

“Hii inalenga kuhakikisha tunapata bidhaa ya thamani bora na itakayonunuliwa haraka katika soko,” anasema afisa mmoja wa kampuni hiyo.

“Ingawa idadi kubwa ya wasimamizi wa kampuni nyingi za kigeni za majani chai eneo la Rift Valley hawataki kufichua madhara ya uchumaji kwa mashine, baadhi yao wanakubali kuwa mbinu hiyo ya kisasa imechangia kushuka kwa ubora majani chai. Mbinu hiyo ya uchumaji imeshusha hadhi ya Kenya kama kitovu cha majani chai meusi na bora zaidi,” anasema.

Henry Omusire, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa KPAWU anataka serikali kuondoa hatua zozote ambazo zinaweza kushusha ubora wa majani chai ya Kenya.

Kulingana na viongozi wa vyama vya kutetea masilahi ya wafanyakazi wa mashamba ya majani-chai, uchumaji kwa mashine utaathiri ubora za majani-chai kando na kuchangia idadi kubwa ya wanachama wao kupoteza ajira.

“Kwa muda mrefu, Kenya imejulikana kwa kuzalisha majani chai ambayo hununuliwa kwa bei ya juu katika masoko ya ulimwenguni. Lakini Kenya haijapata manufaa hayo baada ya kampuni za kigeni kukumbatia uchumaji kwa mashine,” akasema Omusire.