Habari Mseto

Kampuni zajitokeza kufadhili Beyond Zero

February 7th, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Kampuni ya kutengeneza simu ya Huawei imechangia katika kampeni ya Beyond Zero kwa kuipa vipakatalishi 50 aina ya Huawei Matebook X Pro.

Kompyuta hizo zitatumiwa wakati wa utoaji huduma katika kliniki za Beyond Zero, alisema mkurugenzi mkuu wa Huawei Kenya, Stone He.

Kulingana naye, zitasaidia katika kuboresha utoaji wa huduma kwa kusajili wagonjwa na kutoa dawa au kuwafuatilia wanapotibiwa.

Kampuni za Nation Media Group na Standard Group pia zimefadhili mpango huo kwa Sh10 milioni na Sh5 milioni mtawalia.

Beyond Zero ni mradi ulioanzishwa na Mama wa Taifa Bi Margaret Kenyatta kwa lengo la kuimarisha afya ya kina mama na watoto kote nchini.

Mpango huo ulianzishwa 2014 kutokana na utambuzi kwamba inawezekana kuzuia vifo vya kina mama na vifo vya watoto.

Huduma za Beyond Zero hutolewa kupitia kwa ushirika kati ya afisi kuu ya mradi huo, serikali za kaunti na washikadau wengine katika sekta ya afya.