Kampuni zatakiwa kuimarisha usiri wa data za wateja

Kampuni zatakiwa kuimarisha usiri wa data za wateja

Na WANGU KANURI

wkanuri@ke.nationmedia.com

Ulinzi wa data ya kibinafsi umekuwa changamoto nchini Kenya huku wataalamu wakiwarai wakuu wa kampuni na mashirika kuhakikisha kuwa wamelinda na kukomesha uenezaji wa data za wateja bila idhini.

Katika kongamano kuhusu mustakabali wa teknolojia mwaka huu lililoandaliwa na Muungano wa Kuchambua na Kudhibiti Sera za Habari, Teknolojia na Mawasiliano nchini Kenya (KICTANet), wadau katika sekta ya teknolojia walizitaka kampuni kueneza hamasisho kuhusu umuhimu wa ulinzi  wa usiri wa data.

Bi Kui Kinyanjui, Mkuu wa Kudhibiti Sera za Umma katika kampuni ya mawasiliano ya Safaricom, alisema yamkini asilimia 40 ya wateja huhisi kuwa data zao hazijatumiwa kwa kufuata maadili.

Naye Bi Mercy Ndegwa, Mkurugenzi wa Sera za Umma katika Afrika kaskazini na kati wa mtandao wa kijamii wa Facebook, aliwaeleza walioshiriki kuwa ulinzi wa data ni jukumu la kila mwanadamu.

Kwa kutumia mtandao wa kijamii wa Facebook kama mfano, Bi Ndegwa alisema kuwa Facebook humpa mtumizi mamlaka ya kujilinda na kuwadhibiti watu wengine.

“Watumiaji data wanapaswa kulindwa. Hii italazimu mashirika kufahamu na kuhakikisha kuwa kanuni za ulinzi wa data zimeafikiwa na kueleweka,” akasema Bi Immaculate Kassait Kamishna, Kamishna wa Ulinzi wa Data nchini.

Vile vile, wakuu katika mashirika walitakiwa kuhakikisha kuwa wamepewa idhini wanapochukua data za watu. Ili kuhakikisha kuwa kampuni na mashirika yamelinda data walizopokea, yalitakiwa kuwaeleza wenye data hizo jinsi data zao zitatumika, jinsi zitahifadhiwa na pia ni nani atakayepewa ujumbe ulioko kwenye data hizo.

“Ujumbe na watu si bidhaa. Tunapaswa kuthamini na kuwa na utu. Lazima tuzilinde data za watu za kibinafsi,” akaongeza Bi Kassait.

 

You can share this post!

Serikali yawaonya Waluke na Barasa dhidi ya kujiita...

Matumaini ya Leicester City kusonga mbele katika Europa...