Habari Mseto

Kamwe serikali haitaruhusu kamari kurejea – Matiang'i

July 4th, 2020 1 min read

NA FAUSTINE NGILA

Waziri wa Masuala ya Ndani Fred Matiang’i Ijumaa alisema kuwa serikali kamwe haitalegeza sheria za kamari zilizochangia kufungwa kwa kampuni nyingi za kubashiri matokeo ya michezo mbalimbali mwaka uliopita.

Haya yanajiri huku hisia mseto zikitokea miongoni mwa Wakenya mitandaoni kuhusu iwapo serikali inapanga kurudisha biashara ya kamari kwa kuondoa baadhi ya kanuni ilizoweka.

Dkt Matiang’i, alifafanua kuwa serikali itahakikisha sheria hizo zitaendelea kufuatwa ili kuzima uovu unaotokana na kampuni nyingi za kamari. Alisema hayo alipohutubu katika mkutano na viongozi kutoka Kaunti ya Murang’a jijini Nairobi.

Alifichua kuwa amekuwa akipokea malalamishi kutoka kwa viongozi wa dini na Wakenya kwa jumla wakihofia kuwa huenda sheria mpya kuhusu ushuru wa biashara huenda ikaruhusu biashara ya kamari kurejea.

“Hatutarudi nyuma kuhusu sera hiyo kwa kuwa tunataka uadilifu nchini Kenya. Hatungechukua hatua ya kuzima kamari, vijana wengi wangepotelea kwa magenge ya uhalifu na wizi wa hela. Baadhi ya kampuni zilitoka Ulaya na zilikuwa zinafanya mambo ambayo hayaruhusiwa katika mataifa yao,” waziri huyo alisema kwenye mkutano huo.

“Rais wetu amesisitiza kuhusu jambo hili. Ameelezea umma na kuongoza kama mfano kwa wengine. Kamwe haturudi nyuma.”