Habari MsetoMichezo

Kamworor na Chepkoech wanoa kwenye mbio za Eldoret

February 24th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA mara mbili za mbio za nyika duniani Geoffrey Kamworor na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya wanawake ya mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Beatrice Chepkoech wameonyeshwa kivumbi katika mbio za nyika za kitaifa mjini Eldoret, Jumamosi.

Mfalme wa mbio za kilomita 21 kwenye Riadha za Nusu-Marathon Duniani Kamworor, ambaye alinyakua mataji ya mbio za nyika duniani mwaka 2015 mjini Guiyang nchini Uchina na mwaka 2017 mjini Kampala nchini Uganda, aliridhika katika nafasi ya tano katika mbio hizi za kilomita 10, huku Amos Kirui akitwaa taji kwa dakika 29:50.5.

Taji la wanawake la mbio za kilomita 10 lilinyakuliwa na malkia wa Afrika, Dunia na Jumuiya ya Madola wa mita 5,000 Hellen Obiri, ambaye hakumpa Chepkoech nafasi ya kung’ara. Wakimbiaji sita katika vitengo vyote vinne wanatarajiwa kuunda timu ya Kenya itakayoshiriki Mbio za Nyika Duniani mjini Aarhus nchini Denmark mnamo Machi 30, 2019. Takriban mataifa 60 yatawania ubingwa wa dunia mjini Aarhus ambako Kenya itakuwa ikitetea taji ililopokonya Ethiopia mwaka 2017.

MATOKEO (Februari 23, 2019):

Wanaume (kilomita 10)

Amos Kirui (dakika 29:50.5)

Evans Keitany (29:57.4)

Rodgers Kwemoi (29:59.3)

Richard Kimunyan

Geoffrey Kamworor

Rhonex Kipruto

Wanawake (kilomita 10)

Hellen Obiri (dakika 33:14.9)

Beatrice Mutai (33:24.3)

Beatrice Chepkoech (33:54.7)

Wanaume (kilomita nane)

Samuel Chebole (dakika 24:09.8)

Emmanuel Kiprotich (24:17.7)

Leonard Bett (24:25.0)

Wanawake (kilomita sita)

Beatrice Chebet (dakika 20:02.4)

Betty Chepkemboi (20:31.2)

Jackline Rotich (20:39.9)