Makala

Kanani ya Viazi’ inavyotishiwa na mabadiliko ya hali ya hewa

January 22nd, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

KWA wengi, viazi huwa ni vyakula vitamu sana.

Viazi hutumika kupikia aina nyingi ya vyakula, kama vile vibanzi (yaani chips), pure (yaani githeri) kati ya nyingine.

Ijapokuwa zao hilo ni chakula kitamu kwa watu wengi, hasa walio katika maeneo ya mijini, wengi hawajui chimbuko lake.

Unapotembea katika Kaunti ya Nyandarua, moja ya aina ya vyakula utakavyokumbana navyo ni viazi.

Wenyeji huviita ‘waru’—neno linaloonekana kukubalika kote kote zao hilo linakotumika kama chakula ama kiungo cha kupikia.

Zao hilo lilipata umaarufu mnamo 2023, kutokana na wimbo ‘Rieng Genje’ wa kundi la Spider Clan, kupitia mstari “Cash crop za Nyandarua ni mawaru” (Zao la kibiashara la Kaunti ya Nyandarua ni viazi).

Swali lingine ni: Ijapokuwa maeneo mengi huwa yanakuzwa zao hilo, ni eneo lipi linalolizalisha kwa wingi katika kaunti hiyo?

Majuzi, Taifa Leo Dijitali ilizuru katika kaunti hiyo na kubaini kuwa eneo la Boiman ndilo linalosifika kwa uzalishaji mkubwa wa zao hilo.

Kulingana na wenyeji, eneo hilo hutajwa kama ‘Kanani ya Nyandarua’, kwani wenyeji hukimbilia huko wakati kiwango cha viazi kimepungua katika kaunti hiyo.

Eneo hilo liko katika Kaunti Ndogo ya Gathanji, umbali wa kilomita 20 hivi kutoka mjini Nyahururu.

“Boiman huwa kimbilio kwetu wakati uzalishaji wa viazi unapopungua katika maeneo tofauti katika kaunti hii. Ni eneo lenye udongo wenye rutuba, hali ambayo hutoa mazingira bora kwa ukuzaji wa viazi,” asema Bw Maina wa Kihonge, ambaye ni mkazi wa eneo hilo.

Wakazi kadhaa tuliozungumza nao walirejelea hali ya kiangazi iliyotokea  mwanzoni mwa mwaka wa 2000, wakisema kuwa “huo ndio wakati walipoliita eneo hilo ‘Kanani ya Nyandarua’.”

“Nakumbuka vizuri. Mwanzoni mwa 2000, eneo hili lilikumbwa na mojawapo ya kiangazi kibaya zaidi kuwahi kutokea. Hakukuwa na mazao yoyote. Mifugo walifariki. Watoto hawakuwa wakienda shuleni, kwani wengi wao hawangeweza kusoma kutokana na njaa. Baadhi ya  wale waliokuwa wakifanikiwa kwenda shuleni walikuwa wakizimia kwa sababu ya njaa. Hata hivyo, eneo hili liligeuka kuwa mwokozi kwa maelfu ya wakazi, kwani viazi vilikuwa vikipatikana kwa wingi,” asema Bi Immaculate Wambui, ambaye ni mkazi.

Licha ya mafanikio hayo makubwa, wakazi wanasema kuwa hali inabadilika, na ‘baraka’ zilizokuwepo hapo awali zimeanza kupungua kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi – hali ya hewa.

“Kiwango cha uzalishaji kimepungua, hasa kutokana na ukataji mkubwa wa miti. Ijapokuwa serikali imekuwa ikiendesha juhudi za kukabiliana na ukataji miti kiholela katika misitu kama Aberdares, athari za mabadiliko ya hali ya hewa zinatishia kuligeuza eneo hili kutoka ‘Kanani ya Nyandarua’ hadi katika ‘Misri’,” akasema Bi Wambui.

Hivyo, wakazi wanarai wadau husika kuishinikiza jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira ili kuliokoa eneo hilo dhidi ya kupoteza sifa zake za uzalishaji mkubwa wa viazi.