Kananu aahidi kuunga mkono BBI

Kananu aahidi kuunga mkono BBI

Na CHARLES WASONGA

ANN Kananu Mwenda ambaye amechunguzwa na Kamati ya Bunge la Kaunti ya Nairobi kubaini ufaafu wake kwa kiti cha Naibu Gavana wa Nairobi ameahidi kushirikiana na Idara ya Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) kwa ajili ya kutoa huduma kwa wakazi.

Bw Mwenda pia alisema anaunga mkono ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI) ambao unapedekeza kuwa Nairobi isalie kama Kaunti huru ili wakazi wavune matunda ya ugatuzi.

‘Tunahitaji kuunga mkono NMS ili wakazi wa Nairobi waweze kupata huduma bila tatizo. Tayari asasi hiyo inafanya kazi nzuri haswa katika mitaa ya mabanda ambapo imechimba visima vya maji na kujenga vituo vya zaidi vya afya,” akasema alipofika mbele ya kamati ya uteuzi iliyoongozwa na kiongozi wa wengi Abdi Guyo, ambaye huwa ni Naibu Mwenyekiti.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo ni Spika Benson Mutura ambaye sasa ndiye Kaimu Gavana wa Nairobi baada ya kutimuliwa kwa Mike Sonko mnamo Desembe 17, 2020, maseneta walioidhinisha hoja ya kumtimua.

Bi Mwenda, ambaye ni Afisa Mkuu wa Idara ya Kushughulikia Majanga katika serikali ya kaunti ya Nairobi, pia alisema kuwa atabuni kamati maalum itakayopalilia ushirikiano kati ya Serikali ya Kaunti ya Nairobi na NMS kwa manufaa ya wakazi wa Nairobi.

Bi Mwenda hata hivyo alisema serikali ya kaunti ya Nairobi inakabiliwa na changamoto kadhaa kama vile idadi kubwa ya wafanyakazi, madeni na kucheleweshwa kwa fedha kutoka Hazina ya Kitaifa.

Vile vile, alidai kuwa shida nyingine ambayo ilikuwa ikiwaathiri mawaziri na maafisa wakuu wa serikali ya kaunti ya Nairobi ni vitisho vya kila mara kutoka kwa Gavana wa zamani Mike Sonko.

“Nikiidhinishwa kuwa Naibu Gavana, nitaanzisha mtindo wa utendakazi mzuri na mawaziri pamoja na maafisa wakuu huku nikihimiza uwazi na uwajibikaji kazini. Maafisa wakuu hawatafanya kazi katika mazingira ya vitisho tena kama ilivyokuwa zamani,” akasema alipokuwa akijibu swali kutoka kwa kiongozi wa wachache Michael Ogada.

You can share this post!

Kananu aidhinishwa kuwa Naibu Gavana wa Nairobi

Museveni kifua mbele Bobi Wine akipinga matokeo ya mapema