Michezo

Kane aongoza Spurs kulaza West Brom 1-0 katika EPL

November 8th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

BAO la 150 la fowadi Harry Kane katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) Jumapili limewawezesha Tottenham Hotspur kupiga West Bromwich Albion 1-0 na kutua kileleni mwa jedwali la kipute hicho kwa mara ya kwanza tangu Agosti 2014.

Mechi hiyo ilikuwa na nafasi chache za pande zote kufungana na ilionekana kukamilika kwa sare tasa baada ya kipa Hugo Lloris kupangua kombora la dakika za mwisho kutoka kwa Karlan Grant wa West Brom huku Spurs nao wakipoteza nafasi nyingi za wazi.

Utepetevu wa mabeki wa West Brom mwishoni mwa kipindi cha pili uliwapa Spurs fursa ya kuchuma nafuu na wakafungiwa bao na Kane aliyemwacha hoi kipa Sam Johnstone katika dakika ya 88. Bao hilo lilichangiwa na beki Matt Doherty aliyesajiliwa na Spurs kutoka Wolves mwanzoni mwa msimu huu.

West Brom ambao kwa sasa wamefunga bao moja pekee kutokana na mechi tano zilizopita, sasa wako katika mduara hatari ya kushushwa daraja.

Mwishoni mwa mechi hiyo, kocha Jose Mourinho alisisitiza kwamba Spurs ni miongoni mwa wagombezi halisi wa taji la EPL msimu huu hasa ikizingatiwa jinsi ambavyo wanasoka Harry Winks, Davinson Sanchez na Steven Bergwijn walivyoridhisha katika mchuano huo.

Mbali na siku ya kwanza ya msimu wake wa mwisho kambini mwa Manchester United ambapo kikosi chake kilicheza kabla ya mpinzani yeyote mwingine, hii ni mara ya kwanza kwa Mourinho kuwa kileleni mwa jedwali la EPL tangu Septemba 2017.

Mechi dhidi ya West Brom ilikuwa ya kwanza kwa fowadi Gareth Bale kupangwa kwenye kikosi cha kwanza cha Spurs tangu arejee kambini mwa klabu hiyo ya London Kaskazini mwanzoni mwa msimu huu kutoka Real Madrid.

Ushirikiano kati ya Bale, Kane na Son Heung-min unatarajiwa kuwa tishio kikubwa kwa wapinzani wao katika soka ya EPL na bara Ulaya msimu huu.

Ushindi wa Tottenham unatarajiwa kuwapa motisha zaidi wanapojiandaa kwa sasa kuchuana na Manchester City na Chelsea katika mechi zao mbili zijazo za EPL kampeni za kivumbi hicho zitakaporejelewa baada ya michuano ya kimataifa kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA). West Brom watakuwa wageni wa Manchester United katika mechi yao ijayo ya EPL ugani Old Trafford mnamo Novemba 21.

West Brom ya kocha Slaven Bilic ilijitosa ugani kwa minajili ya mechi dhidi ya Spurs bila ya huduma za wanasoka Branislav Ivanovic na Matheus Pereira wanaougua Covid-19.