Kane ashiba sifa za Mourinho baada ya kubeba Spurs dhidi ya West Brom kwenye EPL

Kane ashiba sifa za Mourinho baada ya kubeba Spurs dhidi ya West Brom kwenye EPL

Na MASHIRIKA

KOCHA Jose Mourinho amesema kwamba fowadi na nahodha Harry Kane sasa ataweza kuvunja kila rekodi kwenye soka ya Uingereza baada ya Mwingereza huyo kupona haraka na kurejea uwanjani.

Marejeo ya nyota huyo yalichochea waajiri wake kucharaza West Bromwich Albion 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Februari 7, 2021.

Mechi hiyo ilimpa Kane jukwaa la kufunga bao lake la 208 akivalia jezi za Spurs na hivyo kufikia rekodi ya ufungaji ya aliyekuwa nguli wa soka ya Uingereza, Bobby Smith. Kane sasa yuko pua na mdomo kufikia rekodi ya Jimmy Greaves ambaye ni mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Spurs.

Awali, Spurs walikuwa wameshindwa kufunga bao katika mechi mbili zilizosakatwa na kikosi hicho bila ya kujivunia huduma za Kane, 27.

Hata hivyo, alishirikiana vilivyo na kiungo Pierre-Emile Hojbjerg na kufungia Spurs bao la kwanza katika dakika ya 54 kabla ya Son Heung-min kuzamisha kabisa chombo cha West Brom ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya 12 jedwalini kwa alama 12, moja pekee mbele ya Sheffield United wanaovuta mkia.

“Kane ni mchezaji spesheli sana kwetu na katika historia ya klabu ya Spurs. Ni miongoni mwa washambuliaji bora zaidi katika ulingo wa soka duniani. Kikosi cha Spurs na timu ya taifa ya Uingereza humtegemea sana. Huo ni ukweli usiofichika,” akasema Mourinho.

“Ana uwezo wa kufunga mabao wakati wowote na kuchangia idadi kubwa ya mabao. Pia ana sifa bora za uongozi na ni kielelezo bora kwa wanasoka wengine chipukizi kambini. Huo ndio ukamilifu wa mchezaji,” akaongeza mkufunzi huyo raia wa Ureno.

Bao la Kane dhidi ya West Brom lilikuwa lake la 13 katika EPL msimu huu. Idadi hiyo ya mabao inawiana na ya Son aliyefunga lake baada ya kupokezwa pasi nzuri na Luca Moura aliyewajibishwa na Mourinho katika nafasi ya Gareth Bale.

Alama tatu zilizotiwa kapuni na Spurs ziliwapaisha hadi nafasi ya nane kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 36, nne pekee nyuma ya mabingwa watetezi Liverpool wanaofunga mduara wa nne-bora.

Spurs kwa sasa wanajiandaa kuwaendea Everton kwenye mechi ya raundi ya tano ya Kombe la FA mnamo Februari 10 kabla ya kuwa wageni wa viongozi wa EPL Manchester City mwishoni mwa wiki. Kwa upande wao, West Bromwich Albion wataalika Man-United kwa minajili ya gozi la EPL mnamo Februari 14, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Papa Francis achagua mwanamke katika baraza kuu

Manchester City waponda Liverpool na kujiweka pazuri kutwaa...