Kang’ata ajitetea kuhusu mchango alioaibishwa na Naibu Rais

Kang’ata ajitetea kuhusu mchango alioaibishwa na Naibu Rais

Na SAMMY WAWERU

SENETA wa Murang’a, Irungu Kang’ata amejitetea vikali kuhusu hafla ya harambee ambapo alionekana akishurutishwa na Naibu wa Rais, William Ruto kuongeza kiwango cha mchango wake.

Hafla hiyo ya mapema mwezi huu Murang’a, kulingana na Bw Kang’ata ilikuwa ya kupiga jeki mgombea mmoja wa kiti cha kisiasa eneo hilo kwa tiketi ya UDA, chama ambacho Dkt Ruto ametangaza kutumia kuwania urais 2022.

Kwenye video iliyosambaa mitandaoni, naibu rais aliskika akimtaka seneta huyo anayewania ugavana Murang’a kuongeza mchango wake ufike Sh100, 000. Aidha, Kang’ata alikuwa ametoa Sh40, 000. Ruto alisema mchango huo “ni mdogo sana ukilinganishwa na hadhi yake”.

“ Si unataka ugavana? Hapana, Sh40, 000 hazitoshi gavana. Acha hiyo, enda tafuta Sh100, 000 ulete, wacha kusumbua sisi. “Ni gavana gani wa Sh40, 000? Enda tafuta pesa,” naibu rais akamweleza, akionekana kumsukuma aondoke jukwaani.

Ni tukio lililozua mdahalo na mihemko mitandaoni, video hiyo ikisambazwa na wachangiaji na watumizi. Baadhi ya viongozi na wanasiasa kutoka Mlima Kenya, walikashifu tukio hilo wakilitaja kama linalodunisha watu wa eneo hilo.

Akizungumza jijini Nairobi, seneta Kang’ata hata hivyo alisema ulikuwa utani wa Ruto na kwamba hakuchukulia tukio hilo kwa uzito. “Mchango wangu ulikuwa kwa hiari, nilijitolea bila kulazimishwa na yeyote,’ akasema, akimtetea Ruto.

“Kufuatia utani wangu na naibu wa rais, silalamiki. Halikuwa tukio linalopaswa kuchukuliwa kwa uzito. ”Bw Kang’ata alisema ni kawaida wanasiasa nyakati zingine kuzua ucheshi na kutaniana. Dkt Ruto amekuwa akishiriki hafla mbalimbali za michango, kama vile harambee za ujenzi wa makanisa.

Vilevile, amekuwa akitoa mamilioni ya pesa kwa makundi ya kina mama na vijana, chini ya nembo yake ya hastla akilenga kina mama mboga na wahudumu wa bodaboda. Huku wapinzani wake wakimtaka aelezee anakotoa pesa anazosambaza, baadhi ya maeneo yameshuhudia vurugu wanaofadhiliwa wakilalamikia kukosa kupokea fedha anazotoa.

Naibu rais amekuwa akitumia mbinu za mchango na kuinua makundi ya watu wanaoendeleza biashara kufanya kampeni kusaka kura kuwania urais mwaka ujao. Ziara yake eneo la Kondele, Kisumu Novemba ilikumbwa na ghasia, msafara wake ukivamiwa kwa kile idara ya polisi ilidai “kuchochewa na watu kutoelewana kugawa pesa alizotoa”.

Wapinzani wake, wakiongozwa na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga wamekuwa wakishinikiza awe wazi kuhusu kiini cha mamilioni anayosambaza kwa umma. Aidha, wamekuwa wakimhusisha na sakata za ufisadi na ufujaji wa mali ya umma.

You can share this post!

Wakenya wachanjwe, lakini si kwa vitisho – Amnesty...

Mbunge apendekeza kutathminiwa kwa sheria za uchaguzi...

T L