Kang’ata amtaka Matiang’i arekebishe notisi yake ya saa za kafyu

Kang’ata amtaka Matiang’i arekebishe notisi yake ya saa za kafyu

Na MWANGI MUIRURI

SENETA wa Murang’a, Irungu Kang’ata amemtaka Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i arekebishe notisi katika gazeti rasmi la serikali kwa sababu kwa kiasi fulani inakinzana na tangazo la Rais Uhuru Kenyatta kuhusu kafyu ya kitaifa.

Katika chapisho la Machi 29, 2021, Dkt Matiang’i aliandika kwamba kafyu kote nchini inaanza saa mbili usiku.

Taarifa hiyo ya Matiang’i inakinzana na tangazo la Rais Kenyatta ambaye alitangaza kwamba kafyu iliyobadilika ni ile tu ndani ya mduara wa kaunti tano ambazo aliziliorodhesha kama kitovu kikuu cha maambukizi ya Covid-19 nchini na hivyo basi akazifunga kutangamana na nyingine 42.

Tangazo hilo la Rais la Machi 26 lilijumuisha kaunti za Nairobi, Kajiado, Nakuru, Machakos na Kiambu kama zilizotengwa na kafyu ndani ya mduara huo ikawekwa ianze kutekelezwa saa mbili usiku.

Bw Kang’ata ambaye ni wakili akiongea na kituo cha redio cha Gukena Alhamisi asubuhi, amesema kuwa Kenya ni taifa la kufuata sheria ambazo zimeandikwa kama mwongozo wa kukata kwa maana ya kuamua kesi.

“Notisi hiyo ya Matiang’i kwa sasa ndiyo mwongozo rasmi wa kisheria na ndiyo inafaa kutumiwa nyanjani na maafisa wa polisi. Katiba ya Kenya katika kipengele cha 135 inasema kuwa “maamuzi ya Rais katika kutekeleza majukumu yake yote ya kikatiba katika mwongozo wa Katiba inayotumika kwa sasa yanafaa kuwa ndani ya maandishi yaliyo na nembo ya kitaifa na sahihi yake rasmi.”

Bw Kang’ata anasema kuwa huwezi ukaepuka adhabu ya notisi ya Matiang’i kwa msingi kuwa Rais alisema kwa mdomo wake tena hadharani kwamba kafyu ni ya saa nne usiku nje ya kaunti zile tano ambazo zimetengwa.

“Maandishi rasmi ya kutumika ni yale yako katika notisi ya Dkt Matiang’i na kabla ya irekebishwe, unafaa kukamatwa kwa kukiuka kafyu kote nchini saa mbili ikipita,” amesema Bw Kang’ata.

Katika hali hiyo, leo Alhamisi ikiwa ni siku ya 10 tangu Dkt Matiang’i atoe chapisho hilo, usishangae kukamatwa na maafisa wa polisi mwendo wa saa mbili na dakika moja jioni kwa makosa ya kukaidi kafyu hiyo ya Covid-19.

Katika mitandao ya kijamii, wengi hata maafisa wa polisi wanazidi kuichangamkia taarifa hiyo ya Dkt Matiang’i kwa kejeli na ucheshi.

Yupo afisa aliyetumia ucheshi akisema kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii kwamba: “Dkt Matiang’i anajali maslahi yetu. Anaonekana kuelewa kuwa mshahara wetu ni duni na ametuundia mpango wa kuvuna kutoka kwa raia wasiojua sheria ya kafyu imebadilishwa kimyakimya.”

Afisa mwingine alitaja hitilafu hiyo kuwa kiini cha uchochezi wa ulevi.

Kuna baadhi ya raia walizindua mjadala wa kisheria wakihoji kama ikiwa watakamatwa kwa msingi wa ilani hiyo ya Dkt Matiang’i na wawasilishwe mahakamani wangejitetea namna gani.

“Nikikamatwa saa mbili na dakika kadha nje ya Kaunti zile tano kwa kukiuka kafyu ambayo Rais aliniambia inafaa kunianzia saa nne usiku na upande wa mashtaka uwasilishe notisi ya Dkt Matiang’i kama ushahidi wao, mimi nitakubaliwa kumuita Rais kama shahidi wangu aseme makossa ya kunipotosha nivunje sheria ni yake?” akahoji mwingine.

You can share this post!

Zeddie Lukoye awasilisha barua Waislamu wamsamehe kwa...

Jinsi Taa Steriliser inavyoweza kufanya pesa, vifaatiba na...