Kang’ata awataka Wakenya wawe makini kipindi hiki idadi ya visa vya Covid-19 ikipanda kwa kasi

Kang’ata awataka Wakenya wawe makini kipindi hiki idadi ya visa vya Covid-19 ikipanda kwa kasi

Na MWANGI MUIRURI

SENETA wa Murang’a Bw Irungu Kang’ata amejitokeza Alhamisi na kuelezea kuwa amekuwa hoi akiuguza ugonjwa ambao hakuufichua.

Ameambia Taifa Leo kwa simu kwamba “kuanzia Februari 16 nilijipata na ugonjwa ambao umeniweka nje ya jukwaa la hadharani.”

“Nataka ijulikane tu kwamba sijakuwa katika hali njema kiafya lakini Mungu ni mwema,” amesema Kang’ata.

Bw Kang’ata akifahamika vyema kwa kuchangia mijadala katika mitandao ya kijamii na pia kila siku kutoa dokezi za shughuli zake kisiasa kwa wanahabari, katika kipindi hicho cha karibu wiki mbili, amekuwa ‘mteja wa kuadimika’.

“Licha ya kuwa sijapata nafuu kabisa, niko na amani ya kiafya na kuwa nimenusurika makali ya kuugua moyo wangu ukibakia kumshukuru Mungu kwa wema wake wa kuniponya,” amefafanua.

Amewataka Wakenya wazingatie masharti ya Wizara ya Afya ya kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 akisema kwamba wimbi la tatu limekuja na makali zaidi hivyo wanafaa kuchukua tahadhari kuu.

Alisema sekta za uchukuzi wa umma, burudani na ujasiriamali sokoni na pia makongamano ya umma katika jamii ni baadhi tu ya vichocheo vya kusambaa kwa Covid-19.

Kabla ya kutoweka ghafla kutoka jukwaa la mikutano hadharani, Seneta Kang’ata alikuwa akitekeleza misururu ya mikutano ya maendeleo na siasa mashinani katika Kaunti ya Murang’a ambapo analenga kuwania ugavana 2022.

You can share this post!

Guinea na Mali zafuzu kwa fainali za AFCON kutoka Kundi A

Burkina Faso yawa nchi ya saba baada ya Algeria, Mali,...