Kang’ata sasa akiri ameonja makali ya Covid-19 mara mbili

Kang’ata sasa akiri ameonja makali ya Covid-19 mara mbili

Na MWANGI MUIRURI

SENETA wa Murang’a Bw Irungu Kang’ata sasa amefungua roho na kukiri kuwa ameonja makali ya ugonjwa wa Covid-19 mara mbili sasa katika kipindi cha miezi minane.

“Mara ya kwanza ilikuwa ni Agosti 2020 na tena katika kipindi cha wiki mbili sasa nimejipata mgonjwa wakati huu wa wimbi la tatu ambalo linazidi kutesa hapa nchini kwa sasa,” Bw Kang’ata akaambia Taifa Leo.

Alisema kuwa hilo sio jambo la kawaida na anamshukuru Mungu kuwa amekuwa akimbariki na baraka ya uponyaji katika mapambano hayo mawili na kuibuka mshindi.

Bw Kang’ata aligonga vichwa vya habari Desemba 2020 alipomwandikia barua Rais Uhuru Kenyatta akimuonya kuwa Mpango wa Maridhiano (BBI) eneo la Mlima Kenya ulikuwa hauna ufuasi na ulikuwa na uwezekano mkuu wa kuangushwa na wenyeji katika refarenda.

Bw Kang’ata ambaye alikuwa amekabidhiwa wadhifa wa Kiranja wa Wengi katika Seneti baada ya Seneta wa Nakuru Bi Susan Kihika kutimuliwa kwa kuwa mfuasi sugu wa Naibu Rais Dkt William Ruto akajipa umaarufu ghafla.

Aliingia katika majukumu yake mapya kama kiranja kwa kuandaa mikutano ya kuwaadhibu waasi ndani ya Seneti ambao makosa yao wengi wanahisi “yalikuwa tu kuegemea upande wa Dkt Ruto kisiasa”.

Lakini hata akiwa kiranja aliyeaminika kuwa mfuasi wa Rais na siasa za Handisheki, shaka za uaminifu wake zilkikuwa zikichipuka hasa alipotisha kuwa Jubilee ingejiondoa kutoka Handisheki na BBI iwapo kiongozi wa ODM Raila Odinga hangesaidia Rais Kenyatta kupitisha mswada wa ugavi pesa zakaunti kwa mfumo wa shilingi moja kwa mtu mmoja almaarufu one man one shilling’.

Hata hivyo, baada ya kuandika ile barua kwa Rais akidunisha BBI, naye kichwa chake kikakabidhiwa Katibu Mkuu wa Jubiliee Raphael Tuju na mshirika wake mkuu ambaye ni Naibu Mwenyekiti David Murathe ambao wamejipa nembo sawa na ile ya kinyozi asiyependa kutumia maji akinyoa, na Kang’ata akavuliwa wadhifa huo na kukabidhiwa Seneta wa Kiambu, Kimani Wamatangi.

Bw Kang’ata akiondoka alikejeli kuwa “hata kunipea wadhifa huo wa kuwa kiranja yalikuwa makosa makubwa kwao kwa kuwa mimi kwa muda huu wote nimekuwa mfuasi sugu wa Dkt Ruto na hata mkikumbuka vizuri, mimi ndiye nilikuwa mwasisi wa vuguvugu la Tangatanga.”

Bw Kang’ata alianza kujumuika na Dkt Ruto katika mikutano ya kampeni katika maeneo kadha ya hapa nchini.

Akatoweka ghafla na ni katika hali hiyo ambapo wafuasi wake walianza kuonyesha wasiwasi wao wakiwajibisha vyombo vya habari viwaelezee aliko Bw Kang’ata baada ya kuondoka ghafla kutoka jukwaa la hadhara kwa kipindi cha wiki mbili.

Uvumi ulianza kusambaa kuwa alikuwa ameambukizwa virusi hatari vya corona, hali iliyozua taharuki hasa katika Kaunti ya Murang’a anakolenga kuwania ugavana 2022.

“Ndio nimekuwa mgonjwa sana lakini kwa sasa siko hospitalini, ninaendelea kupata nafuu. Nimepata maambukizi mara mbili sasa, Agosti ya mwaka 2020 na sasa kwa wiki mbili nimekuwa nikiuguza makali yake,” akasema.

Bw Kang’ata amewashukuru wale ambao wamekuwa wakijaribu kumfikia kwa simu kumjulia hali, akisema kuwa “tunafaa kuchukua kila aina ya tahadhari kujikinga na ugonjwa huu.”

Alisema kiuwa akisharejelewa na nguvu zake za kiafya atakuwa balozi wa dhati wa kuhamasisha Wakenya wachukue tahadhari kwa kufuata masharti yote ya kiafya yaliyotolewa kupambana na Covid-19 “lakini pia nikiwapa ushahidi na imani kuwa ukijipata umeambukizwa, unaweza ukapona.”

You can share this post!

Uhuru afunga kaunti 5

Kenya yazoa medali 12 ndondi za Afrika Ukanda wa Tatu...