Michezo

Kangemi Allstars yashindwa kutamba ugenini

May 20th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Kangemi Allstars iliona giza ilipocharazwa mabao 3-2 na Nairobi Stima kwenye mechi ya kupigania ubingwa wa Supa Ligi ya Taifa (NSL) iliyochezewa uwanjani Karuturi Naivasha.

Nayo Wazito FC iliidhalilisha Green Commandos kwa magoli 6-0 na kuendelea kusalia kileleni kwenye msimamo wa kipute hicho. Kwenye mfululizo wa michuano hiyo, Kibera Black Stars iliilambisha sakafu Thika United ilipolizwa mabao 2-1 uwanjani Thika Stadium.

Nairobi Stima ilipiga hatua na kufikisha alama 67 baada ya kuvuna pointi tatu muhimu kupitia Dennis Oalo aliyepiga mbili safi huku Raphael Asudi akiitingia bao moja.

Kangemi Allstars ilitwaa mabao ya kufuta machozi kupitia Konan Kouassi na Mohammed Anaba baada ya kila mmoja kutikisa wavu mara moja. Mabao ya Kibera Black Stars yalifumwa na Wilson Njuguna huku Peter Mwaniki akiifungia Thika United bao la pekee.

”Dah! Nimegundua ligi zote kubwa na ndogo mambo ni moto,” kocha wa Ushuru, Ken Kenyatta alisema na kushukuru wachezaji wake baada ya kuponda St Josephs Youth mabao 2-1.

Nayo Kisumu Allstars ilinasa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coast Stima. Modern Coast Rangers ilitandikwa magoli 3-0 na Bidco United, Eldoret Youth ilibanwa mabao 2-0 na Mafaande wa Kenya Police.