Michezo

Kangemi Ladies kusajili wachezaji sita

June 15th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

INGAWA mlipuko wa virusi hatari vya corona umesitisha shughuli za michezo kote duniani, Kangemi Ladies inasadiki kuwa ingali imara kujituma kiume kukabili wapinzani wao kwenye kipute cha Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza msimu huu.

Kangemi Ladies ilitwaa tiketi ya kufuzu kupandishwa ngazi kushiriki ngarambe hiyo ilipomaliza ya kwanza kwenye mechi za Nairobi West Regional League (NWRL) muhula uliyopita. Kikosi hicho kilinasa tiketi ya moja kwa moja kushiriki kipute hicho maana tawi la Nairobi Mashariki halikuwa na timu ya wanawake.

Timu hiyo chini ya kocha, Loice Karanja na Joseph Orao ilihifadhi taji hilo bila kudondosha mechi yoyote. Wasichana hao walifanya kweli kwenye kampeni za kuwania taji hilo licha ya kupata ushindani mkali kutoka kwa mahasimu wakuu kama Uweza Women, Amani Queens bila kuweka katika kaburi la Carolina For Kibera (CFK).

Vipusa hao waliibuka kidedea kwenye mechi za ngarambe ya NWRL kwa kukusanya alama 30, tatu mbele ya Uweza Women. Walicheza mechi 12 na kufaulu kushinda patashika tisa na kutoka nguvu sawa mara tatu. Nayo Lifting The Bar kati ya vikosi vilivyopigiwa upatu kufanya kweli ilimaliza ya tatu kwa alama 19, moja mbele ya Carolina For Kibera (CFK).

Kangemi Ladies ilitwaa tiketi ya kusonga mbele baada ya kuteleza msimu uliyopita iliposhindwa na Kahawa Queens katika fainali.

Kocha wa City Queens, Derricque Charltone Desh akiongea na wachezaji wake kabla ya kuingia mzigoni kukabili Kangemi Ladies kwenye patashika ya Nairobi West Regional League(NWRL) uwanjani KNH, Nairobi.

”Katika mpango mzima tunalenga kukamilisha zoezi la kusajili wachezaji sita wapya ili kukiongezea kikosi chetu nguvu kwa kuzingatia mechi za ligi ya juu sio kawaida na kipute tulichokuwa msimu uliyopita,” alisema kocha Karanja na kuongeza kuwa wanatamani sana kuona wameanza mechi za mkumbo wa kwanza.

Mwanzilishi na mwenyekiti wake, Caleb Malweyi anasema ”Nashukuru wachezaji wangu kwa kuhifadhi ubingwa wa kipute hicho ndoto yangu kweli imeanza kutimia.”

Pia alisema wachezaji hao walifanikiwa kubeba taji hilo bila kushindwa baada ya kikosi hicho kujumuisha wachezaji chipukizi. Mwaka jana ofisa huyo alinukuliwa akisema ”Imekuwa vigumu kutegemea wachezaji wakomavu maana nyakati nyingi huwa wameshikika kwenye shughuli za kujitafutia riziki na kukosa nafasi ya kushiriki michezo ipasavyo.”

Kangemi Ladies inajumuisha wachezaji kama: Lydia Asiko, Cynthia Kagoli, Emily Rioba, Lucy Kadzo, Salome Drailer, Sorophine Ajiambo, Mary Taifa, Moureen Atieno, Jemimah Ayako, Fasila Adhiambo, Dorothy Akinyi, Faith Awour, Viola Atieno na Irene Auma.

Kangemi Ladies itajiunga na wapinzani kama Mukuru Talent Academy, Moving The Goalpost (MGT) United, Mombasa Olympics, Limuru Starlets, Sunderland Samba na Joylove FC.