Michezo

Kangemi Ladies wabomoa City Queens

July 15th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya City Queens ilibebeshwa kapu la magoli 8-0 na Kangemi Ladies kwenye patashika ya kukunja jamvi ya kampeni za kuwania taji la Nairobi West Regional League (NWRL) msimu huu iliyopigiwa uwanjani KNH, Nairobi.

Kangemi Ladies ya kocha, Loice Karanja na Joseph Orao iliyokuwa inajivunia kutwaa taji hilo ikiwa imebakisha mechi moja, ilitandaza soka safi na kufaulu kuhifadhi kombe hilo bila kushindwa.

Vigoli hao walionyesha ustadi wao dimbani na kuzoa mafanikio hayo kupitia Dorothy Akinyi aliyejaza kimiani magoli manne huku Fasila Adhiambo na Sorophine Ajiambo kila mmoja akitikisa wavu mara mbili.

Baada ya ufanisi huo Kangemi Ladies inajiandaa kushiriki mpambano wa fainali kutafuta malkia wa kipute hicho Mkaoni Nairobi ambapo mshindi atajipatia nafasi ya kushiriki mechi za mchujo kupigania tiketi ya kupandishwa ngazi msimu ujao.

”Bila shaka nashukuru wachezaji wangu kwa ufanisi huo bila kusahau mashabiki wetu,” kocha Joseph Orao alisema.

Nayo Amani Queens ilizimwa kwa mabao 2-1 na Uweza Women kwenye mchezo uliochezewa Uwanjani Woodley Kibera, Nairobi. Uweza Women ambayo ni kati ya vikosi vilivyotifua kivumbi kikali msimu huu, ilipata ushindi huo baada ya Cynthia Akoth kucheka na wavu mara mbili.

Naye Vincecia Mandela aliitingia Amani Queens bao la kufuta machozi. Kwenye mechi nyingine, Carolina For Kibera (CFK) ilitoka sare tasa dhidi ya Lifting the Bar.