Michezo

Kangemi Ladies walenga juu zaidi

July 25th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

BAADA ya Kangemi Ladies kuhifadhi taji la Nairobi West Regional League (NWRL) inajiandaa kujituma mithili ya mchwa kwenye kutafuta ubingwa wa kipute hicho Kaunti ya Nairobi ili kufuzu kushiriki mechi za mchujo.

Kangemi Ladies ya kocha, Joseph Orao akisaidiana na Loice Karanja ilihifadhi taji hilo bila kudondosha mchezo wowote.

Kina dada hao walifanya kweli kwenye kampeni za kufukuzia ubingwa huo licha ya kukutanishwa na upinzani mkali kutoka kwa mahasimu wakuu Uweza Women, Amani Queens bila kuweka katika kaburi la Carolina For Kibera (CFK).

”Bila shaka tunasubiri mchezo wa fainali kubaini nani malkia wa kipute cha msimu wa 2018/2019 baina yetu na mabingwa wa Nairobi East Regional League (NERL),” kocha Orao alisema na kuongeza kuwa hawana budi mbali lazima wajipange vizuri kukabili wapinzani wao.

Kangemi Ladies iliibuka kidedea kwenye mechi za ngarambe ya NWRL kwa kukusanya alama 30, tatu mbele ya Uweza Women.

Vigoli hao walicheza mechi 12 na kufaulu kushinda patashika tisa na kutoka nguvu sawa mara tatu. Nayo Lifting The Bar kati ya vikosi vilivyopigiwa upatu ilifanya kweli ilipomaliza nafasi ya tatu kwa kuzoa alama 19, moja mbele ya Carolina For Kibera (CFK).

Mwanzilishi na mwenyekiti wake, Caleb Malweyi anasema ”Nashukuru wachezaji wangu kwa kuhifadhi ubingwa wa kipute hicho ndoto yangu kweli imeanza kutimia.” Pia alisema wachezaji hao walifanikiwa kubeba taji hilo bila kushindwa baada ya kikosi hicho kujumuisha wachezaji ambao ni wanafunzi wa shule.

Mwaka jana ofisa huyo alinukuliwa akisema ”Imekuwa vigumu kutegemea wachezaji wakomavu maana nyakati nyingi huwa wameshikika kwenye shughuli za kujitafutia riziki na kukosa nafasi ya kushiriki michezo ipasavyo.”

Anne Conguge (kulia ) wa Uweza Women, amkingia mwenzake wa Carolina for Kibera katika patashika ya kipute cha Nairobi West Regional League (NWRL) ugani Woodley Kibera, Nairobi. Picha/ John Kimwere

Vigoli hao ambao ni wanafunzi katika Shule ya Upili ya Dagoretti Mixed wanatarajiwa kushiriki fainali za kitaifa za michezo ya Shule zitakazopigiwa katika Kaunti ya Kisumu wikendi hii (Jumamosi).

Dagoretti Mixed ilitwaa tiketi ya kushiriki fainali za kitaifa mwaka huu baada ya kufanya kweli katika fainali za Mkoa wa Nairobi. Wasichana hao watawakilisha Mkoa wa Nairobi baada ya kuibuka malkia bila kupoteza mechi hata moja.

Wachezaji wataongozwa na kocha huyo ambaye huwafunza wakishiriki mechi za Ligi. Kocha huyo anadai hawana la ziada mbali watakuwa kazini kupigana kwa udi na uvumba amza kuu ikiwa kuibuka kati ya nafasi mbili za kwanza ili kushiriki fainali za ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati zitakazopigiwa nchini Tanzania.

Katika fainali ya Mkoa wa Nairobi, Dagoretti Mixed ilibomoa Olympic Mixed kwa mabao 7-1.

Kwenye nusu fainali, Dagoretti Mixed ilifunga Huruma Girls mabao 3-0 nayo Olympic Mixed ilivuna mabao 6-1 dhidi ya Maina Wajingi Girls. Katika robo fainali Dagoretti Mixed ilijivunia kupepeta Kariobangi North kwa magoli 7-1.

Kwenye ratiba ya fainali za kitaifa, Dagoretti Mixed imepangwa Kundi A linalojumuisha Nyakach Girls (Nyanza one), Itigo Girls (Mkoa wa Bonde la Ufa) na Karugwa Girls (Mkoa wa Mashariki). Nalo Kundi B: Kwale Girls (Pwani), Gezero Girls (Nyanza Two), Bishop Njenga Girls (Magharibi) pia Njambini Girls (Mkoa wa Kati).

Kangemi Ladies ambayo ndiyo Dagoretti Mixed inashirikisha wachezaji: Lydia Asiko, Cynthia Kagoli, Emily Rioba, Lucy Kadzo, Salome Drailer, Sorophine Ajiambo, Mary Taifa, Moureen Atieno, Jemimah Ayako, Fasila Adhiambo, Dorothy Akinyi, Faith Awour, Viola Atieno na Irene Auma.