Michezo

Kangemi Ladies wazidi kudhihirisha makali yao

May 7th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Kangemi Ladies iliendelea kujiongezea matumaini ya kusonga mbele iliponasa pointi sita muhimu baada ya kushiriki mechi mbili za kufukuzia taji la Nairobi West Regional League(NWRL) msimu huu.

Wasichana hao ambao hutiwa makali na kocha Loice Karanja walikandamiza Uweza FC kwa mabao 3-0 kisha kutwaa mabao 3-1 mbele ya Lifting the Bar.

Wachana nyavu hao walishinda Uweza FC na kulipiza kisasi baada ya kuiachia pointi zote tatu walipokosa vyeti muhimu kwenye mechi za mkumbo wa kwanza.

”Tulijaa furaha tele tulipozima Uweza FC na kulipa hatua ya kupokonywa ushindi kwenye mchezo wa utangulizi,” mchezaji wa Kangemi Ladies, Fasila Adhiambo alisema.

Kwenye mchezo wao na Lifting the bar, walifungaji walikuwa Fasila Adhiambo, Sorophine Ajiambo na Drailer Salome waliotikisa wavu mara moja kila mmoja.

Kwenye mchezo wa pili, Fasila Adhiambo alipiga ‘hat trick’ na kubeba Kangemi Ladies kutia kapuni alama zote.

Nayo Amani Queens iliipepeta Lifting the bar mabao 3-0 kupitia Susan Akinyi, Joan Makobe na Ribera Inyanje. Nao Noelah Shikoli alipiga mbili safi huku Mercy Machi akifunga bao moja na kubeba Carolina for Kibera kulaza Kibagare Girls mabao 3-1 huku City Queens ikivuna mabao 3-0 dhidi ya The UoN Queens.