Michezo

Kangemi Ladies yatetemesha ligi

June 18th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

WANASOKA wa Kangemi Ladies walivuna pointi sita nayo Uweza Women ilitwaa alama nne baada ya kila moja kucheza mechi za kuwania taji la Nairobi West Regional League (NWRL) msimu huu.

Drailer Salome alicheka na wavu mara moja na kubeba Kangemi Ladies kuliza Lifting the Bar FC bao 1-0 kisha iliichoma Amani Queens kwa mabao 3-1 kwenye patashika iliyoandaliwa uwanja wa Vetlab Kabete.

Nao wanasoka wa Uweza Women waligaragaza Kibagare Girls mabao 2-1 kabla ya kuteleza na kutoka sare ya tasa dhidi ya Carolina for Kibera.

Kangemi Ladies ya kocha, Loice Karanja ilivuruga wenzao wa Amani Queens na kuwafanya kukosa ujanja dimbani.

Mafanikio hayo yalipatikana kupitia Dorothy Akinyi, Sorophine Ajiambo na Lucy Kadzo walioitingia bao moja kila mmoja.

Uweza Women ilivuna ushindi mbele ya Kibagare Girls pale Mildred Hanisi na Christine Akoth kila mmoja alipotikisa wavu mara moja.

Akielezea kuhusu kampeni za kipute cha msimu huu, kocha wa Uweza Women, Domitila Wangui alishukuru wasichana wake na kusema “Tunataka kufuzu kushiriki mechi ya kupigania tiketi ya kupanda ngazi lakini tuna shughuli zito mbele yetu.”

Kwenye mechi nyingine, Dorcas Vihenda alipiga mbili safi huku sajili mpya Susan Bwibo akicheka na wavu mara moja na kubeba Amani Queens kuvuna mabao 3-1 dhidi ya City Queens.

Kufuatia matokeo hayo, Kangemi Ladies ingali kifua mbele kwa kukusanya alama 20, mbili mbele ya Uweza Women. Amani Queens imefunga tatu bora kwa alama 14.

Kipute hicho kinajumuisha timu nane ikiwemo: Kangemi Ladies, Uweza Women, Amani Queens, Lifting the Bar, The UoN Queens, City Queens, Kibagare Girls na Carolina for Kibera.