Michezo

Kangemi Patriots na Kangemi Ladies wapaa Chapa Dimba

April 7th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Kangemi Patriots na Kangemi Ladies zilitangulia kufuzu kwa fainali za fainali za Tawi la FKF Nairobi West, kitengo cha wavulana na wasichana kwenye michezo ya Chapa Dimba na Safaricom Season Two mwaka huu.

Kila moja ilinasa tiketi hiyo baada ya kufanya kweli kwenye fainali za Kanda ya Westlanda zilizopigiwa uwanja wa Kenya School of Governament (KSG) Lower Kabete, Nairobi.

Timu hizo zitakutana na mabingwa kutoka Kanda ya Lang’ata, Dagoretti na Starehe kutafuta washindi wawili kwa kila kitengo kuwakilisha Tawi hilo katika fainali za Mkoa wa Nairobi. Fainali za Mkoa wa Nairobi zitajumuisha washindi wa nafasi mbili za kwanza kwa kila kitengo kutoka Tawi la Nairobi West na Nairobi East.

Wachezaji wa Kangemi Ladies wakipasha misuli kabla ya kushuka dimbani kukabili Kibagare Girls kwenye mechi za Kanda ya Westlands kuwania Chapa Dimba na Safaricom Season Two Tawi la Nairobi West. Timu hiyo ilishinda bao 1-0 na kufuzu kwa fainali za Tawi hilo. Picha/ John Kimwere

Kangemi Patriots ilibeba tiketi hiyo ilipozaba Kenya School od Government (KSG) Ogoga kwa mabao 3-0 katika fainali. Chini ya kocha, Allan Shibenga ilivuna ufanisi huo kupitia juhudi zake Daniel Gitau aliyetikisa wavu mara mbili huku Samson Obayi aliitingia bao moja.

Kuelekea fainali, Kangemi Patriots ilichoma Young City kwa mabao 3-1 kisha ilituzwa ushindi wa mezani mabao 2-0 baada ya wapinzani wao Gachie FC kuingia mitini. Nayo KSG Ogopa ikiongozwa na kocha, Samuel Njoga mwanzo ilitoka nguvu sawa mabao 2-2 dhidi ya WYSA United kabla ya kuichoma kwa mabao 3-2 kwenye mchezo wa pili na kunasa tiketi ya fainali.

Naye kocha, Joseph Orao aliongoza Kangemi Ladies kudunga Kibagare Girls bao 1-0 kisha kutoka sare tasa na wenzao hao kwenye mchezo wa marudiano na kufuzu kushiriki fainali za Tawi hilo.