Habari za Kitaifa

Kang’ethe anayedaiwa kuua mpenziwe ‘majuu’ alia kuteswa gerezani

March 14th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MSHUKIWA Kevin Kang’ethe anayetakiwa nchini Amerika kufunguliwa mashtaka ya kumuua mpenzi wake, amelalamika anateswa ndani ya gereza la Industrial Area.

Anadaiwa kumuua Margaret Mbitu kati ya Oktoba 30 na Novemba 4, 2023.

Bw Kang’ethe alidai haki zake zimevunjwa kwa kunyimwa fursa ya kuwasiliana na watu wa familia yake.

Pia alidai hapokei chakula ipasavyo.

Alidai ananyimwa fursa ya kuzugumza na wakili wake.

Mshukiwa huyo alidokeza hayo Jumatano alipofikishwa mbele ya hakimu mkuu Lucas Onyina kueleza korti ikiwa amemwajiri wakili mpya kumtetea baada ya kuwatimua mawakili wawili waliokuwa wanamwakilisha tangu akamatwe Januari 2024.

Bw Kang’ethe alimfahamisha Bw Onyina kwamba amefaulu kumteua wakili John Maina Ndegwa kumtetea katika kesi inayomkabili.

Bw Kang’ethe anapinga ombi la serikali ya Amerika arudishwe Massacheussets, jimbo la California kujibu mashtaka ya kumuua Margaret.

Mshukiwa huyo wa mauaji ameomba muda wa siku 21 kuwezesha wakili Ndegwa kusoma na kung’amua yaliyomo kwenye ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuhusu kusafirishwa kwake hadi Amerika.

“Naomba unipe muda wa siku 21 niweze kusoma, kuelewa na kujibu mawasilisho ya DPP kwamba nirejeshwe Amerika kujibu mashtaka ya mauaji,” Bw Kang’ethe alimsihi Hakimu Mkuu katika Mahakama ya Milimani Lucas Onyina.

Kwa upande wake, Bw Ndegwa alisema alipokea maombi ya kumtetea Bw Kang’ethe Jumatano asubuhi na anahitaji muda wa siku 21 kusoma na kutathmini yaliyomo katika ombi la DPP.

Bw Kang’ethe alidai amekuwa kizuizini kwa muda ulioombwa na DPP wa siku 30.

“DPP aliomba nizuiliwe kwa siku 30 polisi wakamilishe uchunguzi. Siku 30 ziliyoyoma Februari 29, 2024. Sasa ninazuiliwa kinyume cha sheria katika gereza la Viwandani,” Kang’ethe alilalama kupitia kwa wakili Ndegwa.

Mahakama ilikumbushwa Bw Kang’ethe alijitilia kitumbua chake mchanga alipotoroka kutoka kituo cha polisi cha Muthaiga.

Akitoa uamuzi Bw Onyina alikubali Bw Ndegwa kutumia siku 21 kusoma na kuwasilisha majibu ya kupinga ombi la DPP kwamba Bw Kang’ethe arudishwe nchini Amerika.

Pia aliagizwa awasilishe hati ya kiapo kuhusu kupinga kuachiliwa kwa dhamana kwa Bw Kang’ethe.

Hakimu aliamuru Bw Kang’ethe aendelee kuzuiliwa katika gereza la Industrial Area hadi Aprili 4, 2024 atakaporejeshwa kortini.