Makala

Kanisa Katoliki lamkubali padri wa mahubiri ya ‘Rap’

March 24th, 2024 3 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

PADRI Paul Ogalo almaarufu Padri Masaa au Sweet Paul, wa Jimbo Katoliki la Homa Bay aligonga vichwa vya vyombo vya habari mwaka 2018 kutokana na mtindo wake wa kipekee wa kuhubiri Injili na kuimba kwa mtindo wa ‘rap’ ambao ni wa kufokafoka.

Padri huyo alisema mbinu hiyo yake ilikuwa ina mchango mkubwa katika kuwavutia vijana kuja kanisani ili apate fursa ya kuwahubiria wayaasi matendo maovu ya kidunia na badala yake kujitolea kuishi maisha ya Imani thabiti.

Video zake za kufoka ziliposambaa mitandaoni–akiwa amevalia mavazi ya kuigiza mbali na yale wavaayo mapadri–uongozi wa kanisa uliingiwa na wasiwasi kuhusu mwenendo wake.

Alichukuliwa kuwa anaenda kinyume na mafundisho ya Kikatoliki ambayo kimsingi ni ya kihafidhina.

Kutokana na hali hiyo, aliitwa na uongozi wa kanisa na baadaye kusimamishwa kuendesha shughuli za kanisa kwa mwaka mmoja.

Askofu Mkuu Philip Anyolo wa Jimbo kuu la Nairobi, ambaye wakati huo alikuwa askofu wa Homa Bay alisema kanisa lilichukua uamuzi wa kumsimamisha kazi Padri Ogalo kwa muda wa mwaka mmoja ili atafakari namna yake ya kuhubiri.

“Tumemzuia kwa kuhubiri akifoka ili kumpa wakati wa kubadilisha njia zake,” askofu mkuu Anyolo akasema.

Lakini miaka mitano baada ya kurejea hudumani, baada ya marufuku hayo kutamatika, Taifa Jumapili ilimtembelea padri huyo na kufuatilia kwa ukaribu shughuli zake kwa siku mbili katika kituo chake cha kazi cha sasa–Parokia ya Rakwaro, Kaunti ya Migori.

Alisema kusimamishwa kwake hakukuchelewesha azma yake ya kugusa nyoyo za vijana wengi hadi kwa njia ya Kristo kwa ufokaji wake, bali kulimpa ujasiri na nguvu ya kukua.

“Hapana kabisa. Ilinitia nguvu na nimeendelea kutumia mtindo wangu wa kuhubiri baada ya kurudi. Popote ninapoendesha misa, kanisa langu huwa limejaa pomoni. Muziki wangu wa kufoka umenisaidia kuwashawishi vijana kuachana na dawa za kulevya na badala yake kuelekeza fikira zao katika masuala ya haki na kimazingira na kijamii,” Padri Ogalo alisema.

Katika siku yetu ya kwanza, Padri Masaa pamoja na mapadri wengine waliongoza misa katika shule ya Upili ya Wavulana ya St Pius Uriri ambapo zaidi ya Wanafunzi 3,000 wa Kikatoliki (YCS) kutoka Dinari ya Rapogi walihudhuria.

Wakati wa mahubiri, Padri Masaa ambaye ana umahiri mzuri wa Sheng’ alifurahisha walimu na wanafunzi kwa mahubiri yake ya kufokafoka. Misa yote ilijaa msisimko huku akiwavunja mbavu mara kwa mara waumini kwa mahubiri yake ya ucheshi.

Siku iliyofuata, ilikuwa Jumapili. Aliendesha misa katika kijiji cha Kitere kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo. Hali ilikuwa sawa na ilivyokuwa huko Uriri. Kila Mkristo aliyehudhuria misa alikuwa akicheka wakati wa mahubiri ya misa hiyo.

Hapa, mtumishi huyo wa Mungu alisisitiza juu ya hitaji la vijana kujitegemea. Aliwaambia wanafunzi kuwa hilo linaweza kupatikana kwa kukumbatia kilimo. Aliwataka wanaoishi katika nyumba za kupangisha kujitosa katika kilimo kifahamikacho kama Kitchen Gardening ili kijupatia mboga za matumizi yao.

“Tunahitaji kufikiria kwa busara. Wacha tujitegemee. Hatupaswi kuwategemea wazazi wetu wakati wote. Tutumie likizo ndefu vyema, kujihusisha na shughuli kama vile kufuga kuku na wanyama wengine ili tuboreshe maisha yetu. Hebu tuepuke dawa za kulevya kwa gharama yoyote kwa manufaa yetu wenyewe,” Padri Masaa alisema.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu waliohudhuria misa iliyoongozwa na Padri Masaa Jumapili hiyo walifichua kwamba amekuwa chanzo chao cha msukumo wa kuhudhuria ibada kanisani.

“Tunapenda mtindo wake wa kuhubiri. Tunaburudika na kucheka kote. Ni vigumu sana kupata uchovu wakati anatuhubiria,” Peris Suswa, mwanafunzi wa Rongo alisema.

Maoni yake yaliungwa mkono na mwenzake Brian Nyachae.

Askofu Michael Odiwa, anayeongoza Jimbo Katoliki la Homabay alisema hakuna ubaya wowote na mtindo wa uhubiri wa Padri Ogalo mradi tu unafanywe kwa kuudhibiti

“Kanisani, siku zote tumekuwa mabingwa wa kuwashirikisha vijana. Kwa hiyo, wakati mapadre wangu wanafanya hivyo, hili ni jambo ambalo linakaribishwa. Lakini ukiona sehemu fulani ukienda nje ya nchi utagundua kuwa kila mchungaji, anahitaji maandalizi. Ikiwa yeye ni mhudumu ambaye hajajitayarisa jinsi ya kuwashughulikia vijana, hatapata matunda. Lakini yule ambaye amejitayarisha kila wakati kama wanaofanya hivyo kwa njia zinazotoa elimu sawia kwa vijana, wanakaribishwa,” Askofu Odiwa alisema.

Padri Ogalo ni mwanamazingira. Anapenda kutunza asili. Katika parokia zote alizofanya kazi, anahakikisha kwamba mazingira ni safi na miti mingi imepandwa ili kupata mahali pema pa kuishi.

Amerekodi nyimbo chache za injili akifoka na kwa sasa anafanyia kazi albamu nyingine, ambayo anakusudia kuitoa hivi karibuni.

[email protected]