Habari Mseto

Kanisa la ACK kupokea sadaka kwa M-Pesa kuzima ufisadi

February 16th, 2020 1 min read

Na KNA

ASKOFU Mkuu wa Kanisa Anglikana (ACK) Jackson ole Sapit, amefichua mipango ya kanisa hilo kuanza kupokea sadaka kwa njia ya simu ili kuzima ufisadi.

Bw Sapit, ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kushinikiza wanasiasa wazimwe kupeleka pesa za ufisadi kanisani, jana alisema mbinu hiyo itasaidia kuleta uwazi.

Akizungumza katika Kanisa la ACK St Paul mjini Lodwar, Kaunti ya Turkana, Askofu Sapit alisema hatua kubwa zimepigwa kufikia sasa kupambana na ufisadi na akataka asasi zinazohusika zisilegeze kamba.

“Unapoona gavana anakamatwa na kuagizwa asiingie afisini mwake kwa sababu ya ufisadi, inamaanisha nchi inapiga hatua bora,” akasema.

Kwa kawaida huwa ni rahisi wapelelezi kufuatilia matumizi ya pesa kielektroniki wanaposhuku mtu alipata pesa hizo kwa njia zinazokiuka sheria kuliko anapotoa pesa taslimu.

Bw Sapit alisisitiza kwamba kanisa la ACK linapinga wanasiasa kufanya harambee makanisani kwani wale wanaotaka kusaidia kanisa wanafaa kufanya hivyo sawa na waumini wengine bila kutangaza michango yao hadharani.

Alisema vita dhidi ya ufisadi havifai kumhurumia mtu yeyote, na wale wanaokamatwa wabebe misalaba yao wenyewe na akaonya umma dhidi ya kuwasifu watu ambao wanashukiwa kuhusika katika ufisadi.

Wakati huo huo, alionya taifa dhidi ya kuingiza siasa katika mchakato wa Mpango wa Maridhiano (BBI) akisema hatua hiyo itawanyima Wakenya nafasi ya kutoa maoni muhimu.

Alisema wakati umefika kwa Wakenya kupiga hatua kuacha kujadili changamoto zinazowakumba, na badala yake waanze kutoa suluhisho kuhusu matatizo hayo.