Habari

Kanisa la Anglikana Mumias lapiga marufuku mazishi ya wikendi

July 11th, 2019 1 min read

Na SHABAN MAKOKHA

[email protected]

KANISA la Aglikana Dayosisi ya Mumias limepiga marufuku shughuli za mazishi wikendi katika kile limesema ni kuchoshwa na mwingilio wa kauli za kisiasa za mara kwa mara.

Askofu Joseph Wandera alisema Jumatano kwamba makubaliano yamepatikana baada ya kikao na wadau muhimu wa kanisa hilo kwamba mazshi yasiandaliwe Jumamosi na Jumapili katika parokia zote 43 chini ya Dayosisi hiyo.

Wakati huo huo, Askofu alisema mazishi yamekuwa yakiathiri ratiba ya kanisa hasa programu za uchangishaji fedha, nikahi, na ubatizo miongoni mwa shughuloi nyinginezo.

“Mkutano wa Nambale, Kaunti ya Busia mnamo Juni 19, 2019, makubaliano yaliafikiwa kwamba kuna sababu za kuridhisha kwamba mazishi yasifanyike wikendi kutoa fursa makasisi kuhudhuria shughuli nyingine hasa harusi, mikutano ya ushirika na pia kutayarisha mafundisho ya kidini ya kusomwa kila Jumapili, alisema Askofu Wandera.

Sasa Mumias inaungana na dayosisi zingine kutoka kaunti zingine nchini Kenya kupiga marufuku mazishi mnamo wikendi.

Dayosisi hizo ni Mount Kenya South, Nyanza, Maseno North na Nambale.

Hilo linamaanisha waliofiwa wanaweza kutoa maiti mochwari Jumatatu hadi Alhamisi na mazishi yafanyike kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa.