Habari Mseto

Kanisa la pasta anayewachochea watoto kuacha shule kuvamiwa

December 28th, 2018 1 min read

Na CHARLES LWANGA

HOFU imeibuka eneo la Malindi baada ya mbunge wa eneo hilo Aisha Jumwa kutishia kuchochea umma kuvamia kanisa ambalo mhubiri wake anadaiwa kuhubiri mafunzo makali kwa waumini wake, na kupelekea visa vya utovu wa nidhamu kuongezeka.

Bi Jumwa alisema kuwa serikali imezembea katika kulizima kanisa la Good News, linaloongozwa na Pasta Paul Makenzi, alilodai limepelekea watoto kuacha shule.

“Licha ya kukamatwa kama mara tatu na kushtakiwa, pasta huyo bado yuko huru ba anaendelea na kazi yake ya kutoa mafunzo makali kwa watoto wa shule,” Bi Jumwa akasema.

Mnamo Septemba, kanda ya video ambapo watoto wa kati ya miaka sita na 17 walikuwa wakikashifu masomo ilisambaa mitandaoni, jambo ambalo lilisababisha ghadhabu za umma.

Oktoba mwaka uliopita, polisi walivamia kanisa hilo na kumkamata pasta huyo akiwa na watoto 93 kwa kutoa mafunzo makali kwa watoto.