Kimataifa

Kanisa laomba waumini wasisusie uchaguzi wa TZ

November 18th, 2019 2 min read

NA CHRISTOPHER KIDANKA

KANISA Katoliki nchini Tanzania, limetoa wito kwa waumini wake kutosusia uchaguzi wa madiwani na viongozi wa manispaa mbalimbali ambao utafanyika Novemba 23.

Vyama vya upinzani nchini humo tayari vimetangaza kwamba vitasusia uchaguzi huo vikilalamikia kubaguliwa na wawaniaji wao kukosa kuidhinishwa na tume ya uchaguzi.

Mkuu wa kanisa Katoliki nchini Tanzania, Askofu Gervas Nyaisonga aliwatakawaumini Wakatoliki kuheshimu maadili ya kanisa na kushiriki kura hiyo.

Hatua ya vyama vya upinzani kususia uchaguzi huo imezua wasiwasi wa kutokea kwa mzozo wa kikatiba iwapo serikali itatekeleza vitisho vya kuendelea nao bila majina ya wawaniaji wa upinzani.

Vyama ambavyo vimekuwa vikipinga sera za utawala wa Rais John Magufuli viliondoa majina ya wawaniaji wao kutokana na masharti mapya yaliyowekwa na Rais Magufuli ya kupiga marufuku mikutano yote ya kampeni tangu 2015.

Hakuna mkutano wowote wa kisiasa ambao umeandaliwa huku uchaguzi huu wa manispaa ukikaribia.

Askofu Nyaisonga alitoa wito huo alipoongoza sherehe za kuadhimisha miaka 25 ya ukasisi wa Askofu wa Shinyanga, Liberatus Sangu.

Hata hivyo mkuu huyo wa kanisa hilo linalojivunia zaidi ya waumini milioni 10 nchini humo, alishikilia kwamba kususia uchaguzi huo sio suluhu na wawaniaji wote wanafaa washirikiane kutatua changamoto ambazo zilisababisha utata wa sasa kutokea.

Chama cha upinzani cha CUF kilikuwa cha hivi punde kutoa tangazo la kususia uchaguzi huo wiki jana kama njia ya kulalamikia mapendeleo kwa chama tawala cha CCM katika uidhinishaji wa wawaniaji.

Awali, vyama vya Chadema, ACT Wazalendo na NCCR-Mageuzi vilitangaza kujiondoa, hatua ambayo sasa inaipa CCM ushindi wa moja kwa moja hata kabla ya uchaguzi wenyewe kuandaliwa.

Vyama vidogo ambavyo pia havina uwakilishi bungeni vya UPDP, CHAUMA na CCK pia vimejiunga na vingine kususia kura hiyo huku muungano wa vyama vingine bado ukiwa haujatangaza iwapo utashiriki au la.

Uchaguzi huo wa madiwani na viongozi wa manispaa umeonekana kama kipimo cha ubabe wa kisiasa kati ya upinzani na CCM huku mchuano halisi ukitarajiwa mwaka ujao wakati wa kura za Urais na ubunge.

Kilicholalamikiwa na upinzani haswa ni kutoidhinishwa kwa zaidi ya nusu ya wawaniaji wa vyama vya upinzani huku tume ya uchaguzi ikitoa sababu za kutokuwa na elimu ya kutosha na baadhi yao kuwa na ‘historia ya ulevi’.